Waziri azomewa mbele ya Pinda., Wananchi wadai amewatelekeza muda mrefu,....



MBUNGE wa Kiteto (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Benedicti Ole Nangoro jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na wananchi mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Nangoro, alizomewa na wananchi katika mji wa Kibaya wilayani Kiteto mkoani Manyara wakati Pinda na uongozi mzima wa mkoa huo walipofanya ziara ya siku moja kujionea uhalibifu mkubwa uliyofanywa wiki iliyopita kati ya wakulima na wafugaji wa jamii ya Kimasai ambapo watu 10 walipoteza maisha.

Baada ya zomeazomea kuzidi, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliamua kumuokoa Nangoro kwa kumchukua na kumpeleka kwenye gari lake kisha kuondoka eneo la tukio.

Hatua ya wananchi kumzomea Mbunge wao, imekuja baada ya madai kuwa kwa kipindi kirefu amekuwa haonekani jimboni kushughulikia kero zao.

Pia walimtuhumu kwamba kabla ya tukio la mauaji kutokea walimwita lakini hakutokea kwa kile kilichoelezwa kuwa alikuwa na kazi maalumu mjini Dar es Salaam.

Mkutano wa jana, uliitishwa uongozi wa mkoa ili kutoa nafasi Pinda kutoa tamko juu ya mauaji na uharibifu mkubwa uliyotokea baada ya wakulima kupambana na wafugaji wa jamii ya Kimasai wiki iliyopita.

Mmoja wa wananchi hao, Zaina Hassani Chuma, alisema siku zote wamekuwa wakimwita mbunge huyo, lakini amekuwa mgumu kujitokeza kuwasikiliza

“Hatumhitaji mbunge kwa sasa, tulimwita kabla ya hata maafa hajatokea sasa anatafuta nini hapa baada ya kumwona Waziri Mkuu….hatukubali tunataka naye ahojiwe kuhusu maafa yaliyotokea na si vinginevyo”alisema.

“Kama Waziri Mkuu, anataka kushughuhulikia tatizo hili kwa umakini aanze kuwakamata baadhi ya viongozi waliohusishwa na mgogoro huu, tena kwa bahati nzuri wanafahamika vizuri kwa kuchangisha fedha za wafugaji ili wawafukuze wakulima,”alisema.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa mkoa pamoja na Pinda, baada ya kusoma alama za nyakati hawakutoa nafasi kwa Nangora kutoa neon la pole kwa wapiga kura wake.

WAZIRI MKUU
Akizungumza na umati wa wananchi, Pianda alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuna kikundi cha watu wachache walioandaliwa kwa ajili ya kuwaua wenzao na kamwe hakikubaliki

Alisema Serikali haiwezi kuvumili na kwamba Serikali imeagiza kikosi cha Operesheni kutoka makao makuu ya polisi ambacho kitaongozwa na Kamanda Simon Sirro kwa lengo la kuwakamata wahalifu wote.

“Suala hili halivumiliki hata kidogo, Tanzania hatujawa na ubaguzi kiasi hiki,kila mtu ana haki ya kuishi mahali popote ili mradi asivunje sheria…sasa hawa wenzetu wana uchungu gani wa kujiona kuwa wana haki ya kuua wenzao”alisema Waziei Pinda

HIFADHI
Kuhusu kuanzisha kwa Hifadhi ya Emboley Murtangosi,Pinda alisema anapata utata mkubwa baada ya kuelezwa jinsi ilivyoanzishwa na kuagiza suala hilo lirejeshwe kwenye vijiji saba vilivyoanzisha eneo hilo ili kujiridhisha kama walishirikishwa wananchi wote.

Alivitaja vijiji hivyo, kuwa ni Kimana,Nameloko,Ndirigishi,Enguserosidani, Lortepesi,Nhati,na Emarti ambavyo vinadaiwa ndivyo vilivyoanzisha hifadhi hiyo ya jamii.

Alisema ana mashaka huenda hata mihutasari haipo, kitendo ambacho kilimlazimu kuuagiza uongozi wa wilaya na mkoa kutafuta taarifa hizo.

“Napata taabu sana namna ilivyoanzishwa hifadhi hii, nimetembelea eneo hilo kwa helkopta mbona sijaona msitu,bali ni mashamba ya wakulima tu? Nataka mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa, RC mnisaidie kuangalia kama kuna uhalali na mihutasari ya vijiji hivyo saba vilivyoanzisha je walishirikishwa”alihoji Waziri Mkuu Pinda

Hata hivyo,Pinda ameagiza wakulima au wafugaji wote hawatakiwi eneo hilo kutokana na hukumu iliyowahi kutolewa na Mahakama Kuu.

Alisema hawezi kuzungumza nje ya kile kilichoamriwa na mahakama na kwamba kwa sasa wakati viongozi Serikali kuendelea kutafuta uhalali wa hifadhi hiyo

Lakini, kaulili hiyo ilionekana kuwakera wakulima na wafugaji wakisema kamwe haiweze kuwa suluhisho na kuongeza mfugaji wataondoka na mifugo yake na mamilioni ya fedha waliyochangishwa na halmashauri yamefanya kazi gani.

MFUGAJI
Kisioki Mesiaya ambaye ni mfugaji, alisema uongozi wa mkoa na wilaya umewagawa wafugaji fedha nyingi ambazo hadi sasa hazijulikani zimefanya nini.

Naye mmoja wa wakulima ambaye hakutaja jina lake litajwe, alisema kauli ya Pinda imewaweka njia panda kwamba wafugaji wataondoka na mifugo yao na wakulima wataondoka na nini wakati kila mmoja alitegemea rasilimali hizo kuendesha maisha ya kila siku.

“Bado Serikali haijaondoa utata mauaji yataendelea, kwani wafugaji wanadai haki yao mamilioni waliyochanga wataendelea kuwepo humo sisis wakulima nasi tutaelekea wapi ili tuweze kuendesha maisha yetu “alisema mkulina huyo

AGOMEA MASWALI
Katika hatua nyingine, Pinda alikataa kuulizwa maswali na wananchi waliokuwa na nia hiyo, kitendo ambacho kilisababisha manung'uniko makubwa kwa wananchi.
Source: Gazeti la Mtanzania/uswazi

0 comments: