MCHUNGAJI ANTONY LUSEKELO (MZEE WA UPAKO) AKIRI KUKAMATWA NA MADAWA YA KULEVYA

Mchungaji wa Kanisa la Maombezi jijini Dar es Salaam (GRC), Lusekelo Anthony ‘Mzee wa Upako’ amekiri kuwa aliwahi kukamatwa na kuwekwa lupango katika Gereza la Keko, Dar kwa siku 14 akituhumiwa kujihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya ‘unga’, Risasi Jumamosi lina sauti yake.


Akizungumza kwa uso wenye majonzi na siha ya huzuni mwishoni mwa wiki iliyopita kanisani kwake Ubungo- Kibangu, Dar, Mzee wa Upako alisema hawezi kuisahau siku hiyo ambayo shetani aliamua kukunjua kucha zake kumwelekea yeye.
Alisema ishu hiyo ilimkuta mwaka 2005 akiwa tayari mtumishi wa Mungu aliye hai, lakini anachomshukuru Mungu ni kwamba alimsimamia kwa nguvu zote.

MCHEZO MZIMA ULIVYOKUWA
Akizungumzia mchezo mzima ulivyokuwa, Mzee wa Upako alisema siku ya tukio (hakuitaja) akiwa kanisani hapo na waumini wake ghafla walitokea askari polisi ambao idadi yao haikumbuki.
Alipotaka kujua shida yao, walisema wao wanatokea Polisi Central, Dar na walikwenda pale kufanya naye mahojiano na kumpekua kwani alikuwa akihisiwa anajishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya.“Polisi walikuja kanisani wakafanya upekuzi, wakaenda nyumbani  nako wakafanya hivyohivyo kisha wakaondoka zao baada ya kutokuona chochote,” alisema Mzee wa Upako.

POLISI WA INTERPOL WATUMIKA
Mzee wa Upako anaendelea kufunguka: Siku mbili mbele  wakaja wengine, wakasema wao ni Polisi wa Kimataifa (Interpol). Nao wakasema wamekuja kunipekua, lakini wao licha ya kutokukuta chochote walinikamata na kunipeleka Mahabusu ya Gereza la Keko, Dar ambapo nilikaa kwa muda wa kama wiki mbili.

AZITAJA SIKU ZA MAJARIBU
Mzee wa Upako: Hakika zilikuwa ni siku za majaribu kwangu kukamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya, lilikuwa ni jambo ambalo sijawahi kulifanya achilia mbali kuliwaza.

Licha ya kukaa kwa wiki mbili kule mahabusu, Polisi wa Interpol nao walijiridhisha kwamba mimi sifanyi biashara hiyo, wakaniachia huru niendelee kumtumikia Mungu wangu.


AWAGUNDUA WABAYA WAKE
Mchungaji huyo maarufu kwa msemo wake WATASHINDANA, LAKINI HAWATASHINDA aliendelea kusema kuwa aligundua kukamatwa kwake kulitokana na mpango wa siri uliofanywa na baadhi ya wachungaji wenzake (hakuwataja majina) kwa ajili ya kumdhoofisha kiimani.
“Zilikuwa ni mbinu chafu za kunidhoofisha kiimani kutoka kwa baadhi ya wachungaji wenzangu wenye wivu na huduma yangu. Lakini kwa jina la Yesu aliye hai walishindwa, watashindana lakini hawatashinda,” alisema Mzee wa Upako.

AHISI KUONDOLEWA HADHI 
Mzee wa Upako alisema tukio hilo aliliona kama la kumwondelea hadhi katika jamii, hususan kwa waumini wake lakini kwa kuwa yeye ni ‘super charge’ kamwe hawezi kuruhusu imani yake iyumbishwe na hila za muovu shetani.

ANACHOMSHUKURIA MUNGU
Mchungaji huyo alisema baada ya kutoka Keko alimshukuru Mungu kwa vile hakuna chombo chochote cha habari kilichofuatilia juu ya sakata hilo na kwamba gazeti hili (Risasi Jumamosi) linakuwa la kwanza kuandika.
“Nashukuru hakuna chombo chochote cha habari kilichogundua juu ya habari hiyo, ninyi mnakuwa wa kwanza kuijua na hata kuiandika kama mtapenda,” alisema Mzee wa Upako.

APINGA DHANA YA WATUMISHI WA MUNGU KUUZA UNGA
Akizungumzia kwa undani sakata la watumishi wa Mungu kujihusisha na biashara ya unga, Mzee wa Upako alisema:
“Siamini kama kweli kuna watumishi wa Mungu wa hapa Tanzania wanafanya biashara hiyo. Kinachotokea ni kwamba, watu wamekuwa wakiwasingizia watumishi kwa sababu zao.”


Juzi Alhamisi, Risasi Jumamosi liliwasiliana na baadhi ya waumini wa kanisa hilo ambapo walisema mtumishi wao huyo amekuwa akionewa kijicho kutokana na mafanikio yake ya kiroho na kimwili.

“Sisi waumini wa GRC tukisikia lolote baya kuhusu Mzee wa Upako huwa hatushtuki kwa sababu wapo baadhi ya watumishi wa Mungu wanamuonea kijicho kwa sababu ana mafaniko ya kiroho na kiimani,” alisema muumini mmoja bila kutaja jina.
Mwingine alisema nguvu kubwa ya kiroho aliyonayo mtumishi huyo imemfanya aibue maadui wasio na hofu ya Mungu kwa kumpakazia skendo mbalimbali wakiamini akichafuka waumini watamkimbia.

Jumatano iliyopita, paparazi wetu alifika Kituo Kikuu cha Polisi (Police Central), Dar na kuulizia ishu hiyo ambapo afande mmoja alisema anayeweza kujua ni IGP Mstaafu, Omary Mahita ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania. 
Hata hivyo, juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa ziligonga mwamba kufuatia simu yake ya kiganjani kutokupatikana hewani.