RAISI
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi
katika sherehe za maadhimisho ya Miaka 37 ya kuzaliwa kwa chama hicho
zitakazofanyika kitaifa Mkoani Mbeya.
Akitoa
taarifa kwa waandishi wa Habari katika Mkutano uliofanyika katika
Ofisi za Chama hicho Mkoa zilizopo Sokomatola Jijini Mbeya, Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godphrey Zambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Mbozi Mashariki alisema sherehe hizo zinatarajiwa kufanyika Februari 2,
Mwaka huu.
Zambi alisema
maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa Chama cha mapinduzi ambayo
yatafanyika kitaifa Mkoani Mbeya na Raisi Kikwete kuwa Mgeni rasmi
yataanza majira ya saa 12 alfajiri kwa kufanya matembezi ya Mshikamano.
Alisema
matembezi hayo yataanzia katika viwanja vya John Mwakangale (nanenane)
na kuishia katika Ofisi za Chama Mkoa eneo la Sokomatola yakihusisha
Viongozi wa Chama na Wananchi mbali mbali wa Mkoa wa Mbeya na mikoa
jirani.
Aliongeza kuwa baada ya
matembezi hayo Wananchi na viongozi watapata mapumziko kidogo na kisha
kuendelea na sherehe katika Viwanja vya Kumbu kumbu ya Sokoine
zitakazoanza majira ya Saa nane Mchana.
Aidha
mwenyekiti huyo alikipongeza Chama cha Mapinduzi Taifa kwa kuuteua Mkoa
wa Mbeya kuwa Mwenyeji wa Sherehe hizo ambazo hazijawahi kufanyika
Mkoani Mbeya tangu kuzaliwa kwa Chama hicho Mwaka 1977.
Alisema
ni fursa pekee ya wakazi wa Mkoa wa Mbeya ya kukutana na Raisi Kikwete
ambaye ataweza kuwaeleza wananchi mafanikio yaliopatikana Mkoani Mbeya
tangu kuzaliwa kwa Chama hicho hadi sasa.
Aliyataja
baadhi ya mafanikio kuwa ni pamoja na Ongezeko la Vyuo vikuu ambavyo
awali havikuwepo Mkoani Mbeya sambamba na kuimarishwa kwa miundombinu
hususani ujenzi wa barabara za Lami ambazo Mbunge wa Chadema Mbeya
Mjini, Joseph Mbilinyi anadai yeye ndiye amejenga.
Alisema
mafanikio mengine wanayopaswa kujivunia wakazi wa Mkoa wa Mbeya ni
pamoja na sekta ya Elimu, Afya, Maji na Umeme ambapo sehemu kubwa ya
Mkoa wa Mbeya wenye wakazi zaidi ya Milioni Mbili na Wanachama wa chama
hicho zaidi ya Laki tatu wakipata huduma bora za kijamii.
Zambi
aliongeza kuwa kutokana na kufanyika kwa sherehe za maadhimisho ya
miaka 37 ya kuzaliwa kwa CCM Mkoani Mbeya, Mkutano wa Halmashauri Kuu ya
Chama hicho ambao awali ulitarajiwa pia kufanyika Mkoani hapa
umeahirishwa na kuhamishiwa mkoa mwingine ambao haukutajwa.
Wakati
huo huo Mwenyekiti huyo alizungumzia mgogoro unaoendelea ndani ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kwamba CCM haihusika nao kama
baadhi ya watu wanavyodai.
Alisema
Chama cha Mapinduzi hakifurahii migogoro ya vyama vya upinzani kwa
sababu vilianzishwa kwa lengo la kuikumbusha Serikali iliyopo madarakani
pindi inapofanya vibaya au kujisahau katika kufanya shughuli za
kuwaletea Maendeleo Watanzania.
Alisema
hata ndani ya CCM matatizo kama hayo hutokea lakini humalizwa kupitia
vikao halali vya chama na kuendelea na shughuli zake kama kawaida na sio
kukimbilia kwenye vyombo vya habari kutangaziana mabaya.
0 comments:
Post a Comment