Hitilafu za mitambo zaipa Tanesco hasara ya mabilioni ya pesa....



Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema kutokana na hitilafu za mitambo hivi karibuni na kuanguka kwa nguzo kubwa mbili za vyuma kumelisababishia shirika hilo hasara ya Sh. bilioni 1.2 kwa Kahama na Sh. milioni 200 kwa Ubungo.

Hitilafu hizo zilitokea katika vituo vya Sokoine na Ubungo jijini Dar es Salaam.
 
Kadhalika, shirika hilo liko mbioni kufanya mabadiliko ya utendaji kwa wafanyakazi wake waliowazembe kazini hususani sehemu za usimamizi.

Taarifa hiyo ilitolewa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba, wakati akiwaelezea waandishi wa habari hali ya umeme hapa nchini.
 
Mramba alisema hadi sasa Tanesco linadai Sh. bilioni 233, mchanganuo huo ukiwamo Sh. bilioni 129 wanazozidai taasisi za serikali ikiwamo Zanzibar inayodaiwa Sh. bilioni 70, na Sh. bilioni 104 wanaowadai watu binafsi na taasisi za watu binafsi.

“Hivi sasa tumeanzisha kampeni maalumu ya kukusanya madeni ambayo itazihusu taasisi za umma, watu binafsi, viwanda, tunawataka wateja wote waweze kulipa madeni yao mapema iwezekanavyo ili kuepuka usumbufu,” alisema Mramba.

Alisema kampeni hiyo itajumuisha kutoa notisi, kuwataka wateja walipe madeni yao ndani ya muda wa notisi pamoja na kuwakatia umeme watu wote ambao hawajalipa.
 
Kadhalika, Mramba alisema kwa wateja waliolipia umeme mwaka jana wataendelea kuunganishiwa umeme na kueleza kuwa ifikapo Februari mwaka huu, wateja wote watakuwa wameshaunganishiwa umeme.

0 comments: