Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangalla Hatarini Kutimuliwa CCM..

Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangalla yuko hatarini kuvuliwa uanachama wa chama hicho, hatua ambayo endapo itachukuliwa itasababisha apoteze nafasi yake ya ubunge.

Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Nzega mkoani Tabora tayari umemjadili Dk Kigwangalla katika vikao vyake vya Kamati za Usalama na Maadili na Kamati ya Siasa, kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu wa mbunge huyo.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana jioni zinasema baada ya vikao hivyo vilivyofanyika Januari 11 mwaka huu, imeazimiwa kuwa suala la Dk Kigwangalla pamoja na madiwani watano wilayani humo lipelekwe katika ngazi ya CCM mkoa na baadaye taifa.

Dk Kigwangalla jana alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema: “Hata mimi nimesikia taarifa hizo, isipokuwa sijapewa taarifa rasmi. Ila nafahamu kwamba vikao vya chama vilikuwepo na mimi niliitwa ila kama ambavyo nimeshasema siwezi kuhudhuria”.

Gazeti hili lilimtafuta Mbunge huyo machachari kutokana na taarifa yake aliyoitoa kwenye mitandao ya Facebook na Tweeter akieleza kuhusu taarifa za kuwapo mpango wa kumfukuza uanachama.

Kupitia mitandao hiyo Dk Kigangwalla aliandika: “Nimepokea taarifa kuwa madiwani walioungana na wananchi wa Nzega pamoja na mimi kupinga uamuzi wa Baraza la Madiwani kuzigawa pesa kwenye Kata wameadhibiwa na Kamati ya Siasa ya Chama Wilaya ya Nzega, bila kusikilizwa na ilhali miongoni mwa ‘mahakimu’ hawa ni watu waliokuwa wakilalamikiwa na madiwani na wananchi. “

Mbunge huyo aliongeza: “Nimepewa taarifa kuwa mapendekezo ya adhabu dhidi yangu kutoka wilayani kwenda vikao vya juu, ...tena bila kusikilizwa maana nilitoa udhuru, ni kuwa ninyang’anywe kadi ya uanachama wa CCM. Nimeshangazwa sana na kusikitishwa na jinsi chama kinavyoendeshwa Nzega.”

Mbunge huyo alisema anaamini viongozi wakuu wa CCM wanafuatilia kwa karibu suala hilo na watachukua hatua stahiki, huku akisema hatahudhuria tena kikao chochote cha CCM wilayani humo.

“Kama chama hiki kimefika huku, kwamba kuna watu wana nguvu kuliko chama, kwamba wachache wanaweza kuwaonea wengine kwa kuwa wana vyeo na mamlaka ya kufanya hivyo na hakuna wa kuingilia kati na kusema ‘no’, basi sina haja ya kuendelea kupambana,” aliongeza.

Aliendelea: “Nimechoka, sintokata rufaa wala sintolalamika tena. Watekeleze hukumu hiyo. Sintojitetea na sintohudhuria kikao chochote kile kuanzia sasa, nimechoka kupambana na watu wenye nguvu, nimechoka. Ni bora kuwa mnyonge, lakini ukabaki na uhai, uzima, heshima na furaha yako”.

Kauli ya CCM Nzega

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nzega, Amos Kanuda alikiri Dk Kigwangwalla kujadiliwa katika vikao vya chama vya wilaya, ikiwamo Kamati ya Siasa.

 

Alisema makosa ya Mbunge huyo ambayo yalijadiliwa katika kikao hicho ni kufanya mkutano wa hadhara na kuwaporomoshea matusi madiwani wenzake ambao hawakuwa upande wake wakati wakijadili mgawo wa fedha.

Mwenyekiti huyo alisema CCM baada ya kuona mgogoro huo wa madiwani wake unakua, kiliamua kuwajadili watuhumiwa na kwamba uamuzi wa kikao hicho ni siri.

Alisema CCM bado inaendelea kumjadili mbunge huyo na kwamba kikao kingine kitafanyika Februari mosi mwaka huu.

Alisema uamuzi wa kikao hicho utapelekwa CCM Mkoa wa Tabora na wao watalijadili na kupeleka mapendekezo yao chama taifa.

Chimbuko la mgogoro

Mgogoro uliokigawa CCM katika Wilaya ya Nzega, unatokana na tofauti za kimtazamo kuhusu jinsi ya kutumia fedha Sh2.3 bilioni zilizotolewa na Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya Resolute kama kodi ya huduma kwa halmashauri ya wilaya hiyo.

Dk Kigwangalla pamoja na madiwani kadhaa wanapinga kupindishwa kwa azimio la Baraza la Madiwani ambalo lilielekeza fedha hizo zitumike kuanzisha Benki ya Jamii ya Nzega (Nzega Community Bank Ltd - NCB) na Kampuni ya Ujenzi ya Jamii ya Nzega (Nzega Community Construction Corporation Ltd - NCCCL).

Lengo la Kampuni ya NCCCL lilikuwa ni kujenga uwezo kwa kuwa na vifaa vya ujenzi wa barabara za halmashauri na mashine ya uchimbaji wa visima kwa ajili ya huduma za maji.

Hata hivyo, wakati utekelezaji wa azimio hilo ukiwa umeanza, Januari 4 mwaka huu kiliitishwa kikao cha dharura kwa lengo la kubadili maazimio ya awali.

Zamu hii madiwani wakiungwa mkono na uongozi wa CCM wa wilaya walikuja na mpango kwamba fedha hizo zigawanywe kwenye kata, azimio ambalo linapingwa vikali na baadhi ya madiwani wakiongozwa na mbunge huyo.

Baada ya azimio jipya kupitishwa, Dk Kigwangalla aliitisha mkutano wa hadhara na kuwahutumia wananchi na mwishoni mwa mkutano huo wananchi waliazimia kufungua kesi mahakamani kuzuia kutumika kwa fedha hizo.

Ni katika mkutano huo ambapo Dk Kigwangalla anadaiwa kuwatusi baadhi ya madiwani waliokuwa kinyume na yeye, matamshi ambayo yamesababisha kuanzishwa kwa mchakato wa kumvua uanachama.

0 comments: