"2015 Maamuzi Magumu na Makini ni muhimu kwa maslahi ya Watanzania " Dk Slaa;


 KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa, amesema ili nchi iondokane na hali ya umaskini, wananchi wanatakiwa kufanya uamuzi mgumu wa kutoirudisha CCM madarakani, katika uchaguzi mkuu ujao, utakaofanyika mwakani.

Dk. Slaa alisema misingi mibovu ya CCM ndiyo sababu ya nchi kuyumba na kwamba hali hiyo imechangia Tanzania kuwa ya pili kutoka mwisho kwa umaskini barani Afrika, wakati nchi ipo katika nafasi ya pili kwa kuwa na rasilimali nyingi.


Kauli hiyo aliitoa juzi, wakati akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Siasa, katika Wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya, ikiwa ni mwendelezo wa Operesheni M4C Pamoja Daima.

Alisema, endapo wananchi watakubali kuwa na uamuzi mgumu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ikifika 2015 kwa kuipa Chadema nafasi ya kuongoza nchi, basi watambue kuwa wameondokana na hali hiyo ya umaskini.

Aidha, aliongeza kuwa Serikali ya CCM imeacha kufanya kazi za kuwatumikia wananchi, badala yake imekuwa ikieneza uongo kwa umma kuwa Chadema ni chama cha kikanda, ukabila na udini na ndiyo maana waliingiza mamluki ili wakivuruge, lakini kwa hilo wameshindwa na hivi sasa Chadema inasonga mbele.

“Kitu cha kwanza kukifanya pindi tutakapoingia Ikulu 2015 ni kuuza ndege ya Rais pamoja na mashangingi ya wabunge, ili fedha itakayopatikana tuipeleke kwenye shughuli za maendeleo,” alisema.

 
 Dk. Slaa aliwapongeza wananchi kwa kutoa maoni yao ambapo wananchi milioni 3 na laki 3 walitoa maoni yao, huku asilimia 72 wakitaka ardhi ya Tanzania wamiliki wenyewe.
 
 Alisema Chadema, chini ya Mwenyeketi wake, Freeman Mbowe, ilifanya utafiti nchi nzima na kugundua kuwa Watanzania milioni 5.8 hawana shahada za kupigia kura na kuamua kutoa fomu na kuorodhesha majina ya watu wasio na shahada.  
Kwa upande wake, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, aliwataka wananchi kuachana na CCM, kwa kuwa kinawapotezea muda na kama wataendelea kuichagua, wasitarajie kupata maendeleo.
 Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu), aliwaomba wananchi waendelee kumpa kero zao, kwa kuwa jimbo la Kyela lipo likizo, kutokana na Mbunge wa Jimbo hilo, Dk Harrison Mwakyembe, kulitelekeza.

“Ninawaombeni Wanakyela mnipe kero zenu, kwani ninafahamu kwamba mbunge wenu amewatelekeza kwa kufanya shughuli bandarini na kwenye viwanja vya ndege,” alisema.


Sugu aliifananisha Wilaya ya Kyela na shamba darasa au daraja la viongozi kupatia vyeo, lakini wanashindwa kuwaletea maendeleo.

Leo Dk. Slaa anatarajiwa kuhutubia wananchi wa Jiji la Mbeya, katika uwanja wa mikutano wa Ruanda, Nzovwe.

0 comments: