Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema, uswahiba wa
Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru
Kawambwa ndiyo chanzo cha kuporomoka kwa cha elimu nchini.
Dk Slaa alisema hayo jana kwenye Viwanja vya Jojo
Kata ya Santilya, Mbeya Vijijini ikiwa ni siku ya tatu ya Operesheni la
Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), Pamoja Daima.
Alisema Dk Kawambwa hana uwezo wa kuongoza wizara
hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa na Chadema kilishangazwa na
mabadiliko aliyoyafanya Rais Kikwete katika baraza lake huku akimwacha
waziri huyo katika nafasi hiyo.
“Kawambwa ni janga la elimu, hana uwezo. Chadema
tutaendelea kumshtaki kwa wananchi. Mfumo mzima wa elimu nchini
unahitaji mabadiliko, ili kufika huko wanahitajika viongozi wabunifu,”
alisema Dk Slaa huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliohudhuria
mkutano huo.
Aliongeza: “Elimu yetu iko shakani, sasa hivi mwenye shahada mbili anafanana na aliyemaliza darasa la nne la zamani.”
Alisema viongozi wa Serikali na CCM hawana uchungu
kwa kuwa watoto wao wanasoma nje ya nchi hivyo aliwataka wananchi
kuitosa CCM katika kila ngazi ya uchaguzi.
Dk Slaa alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi
kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika
baadaye mwaka huu.
Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi
maarufu kama ‘Sugu’ aliwataka wananchi hao kumchagua mgombea Udiwani wa
Chadema, Elisha Mwandele katika uchaguzi mdogo wa Kata ya Santilya
utakaofanyika mwezi ujao.
“Ninyi wananchi ndiyo wenye mamlaka kwa kila kitu,
nawaombeni mumchangue Mwandele ili awe diwani wa kata hii na mabadiliko
yataendelea nchi nzima ili tutume salamu kwa CCM,” alisema Mbilinyi.
Katika hatua nyingine, Helikopta ‘Chopa’
inayotumika katika ziara hiyo ililazimika kukaa kwa zaidi ya saa mbili
katika uwanja wa Jojo kutokana na mvua na ukungu.
Kabla ya kufika hapo helikopta hiyo ilikuwa
ikitokea Kyela mkoani humo na baadaye hali ya hewa iliporejea katika
hali ya kawaida ziara iliendelea kwa Jimbo la Mbozi, kisha kuelekea
katika Mkoa wa Katavi.
Heche awabana Kinana, Nape
Kutoka Arusha, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema
(Bavicha), John Heche amesema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape wanapaswa kujiuzulu, kutokana na
mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, kuwapuuza na kuwateua
mawaziri waliowaita ni mizigo.
Mkutano huo ambao ulifanyika viwanja vya Ngusero
Kata ya Sombetini, Heche alisema kama viongozi hao, walikuwa wanatoa
kauli za kuwapinga kwa dhati mawaziri mizigo na siyo kuwalaghai wananchi
wanapaswa kuwajibika wao kwa kupuuzwa na mwenyekiti wao.
“Sisi Chadema msimamo wetu upo wazi, hao mawaziri
mizigo, tunajua hawana uwezo lakini CCM haina ubavu wa kuwang’oa,”
alisema Heche.
Kwa upande wake, mwanasheria na Chadema, Tundu
Lissu alisema Watanzania wasitarajie mabadiliko yoyote katika utendaji
wa mawaziri.
Hata hivyo, Lissu alisema kazi kubwa ambayo
wanapaswa kuifanya ni kujitokeza kuandikishwa katika daftari la kudumu
la wapiga kura ili wawe na uwezo wa kupitisha Katiba Mpya na kushiriki
katika chaguzi.
Alisema msimamo wa chama hicho ni kuwa kama
daftari la kura halitafanyiwa marekebisho wanachama wote wa chama hicho,
watasusia kura ya maoni ya Katiba Mpya. Lissu alisema wanajua CCM ndio
inafanya njama za kutoboreshwa daftari la kura kwa kuwa wanajua vijana
wengi wakijiandikisha ndio utakuwa mwisho wa CCM.
Lissu pia alisema, CCM imeshindwa kuongoza ndiyo
sababu imekuwa ikishindwa kusimamia hata rasilimali za nchi, yakiwamo
madini, hifadhi za taifa na mambo mengi muhimu.
Awali, Lissu aliwataka wakazi wa kata hiyo
kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili wamchague mgombea udiwani
wa kata hiyo ya Sombetini kupitia Chadema, Ally Benanga.
“Mgombea wetu ni kijana wenu mnamjua, hivyo kazi ni moja tu kumpa kura siku ya uchaguzi Februari 9 mwaka huu,”alisema Lissu.
Taarifa ya nyongeza na Mussa Juma na Zulfa Mussa, Arusha.
-Mwananchi
0 comments:
Post a Comment