Wanamgambo wa Al Shabaab wenye uhusiano na Al-Qaeda, wamesema kuwa
wamepiga marufuku raia wanaoishi katika maeneo wanayodhibiti kutumia
internet.
Wapiganaji hao wametoa onyo kwa kampuni zote zinazotoa huduma ya internet siku 15 kufunga biashara zao. “kampuni yoyote au mtu yeyote atakayepatikana akipuuza onyo hilo
atajulikana kama mtu anayewafanyia kazi maaduzi zetu, na ataadhibiwa
kulingana na sheria za kiislamu,” ilisema taarifa ya kundi hilo ambayo
ilitumwa kwenye mitandao yake.
Wanamgambo hao hutumia sheria kali za kiisilamu katika maeneo
wanayotawala na kuwakamata watu mara kwa mara kwa tuhuma za kufanya
ujasusi.
Internet hutumiwa sana nchini Somalia, taifa ambalo limekumbwa na vita
vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya miongo miwili, huku kundi hilo
likionekana kuwa kikwazo kikubwa kwa amani.
Kundi la Shebab zamani lilikuwa likitawala katika sehemu kubwa za Kusini
mwa Somalia na Kati, lakini likaondoa wapiganaji wake baada ya
kushindwa na wanajeshi wa Muungano wa Afrika wanaopambana nao. Majeshi
ya Afrika wakiwemo wanajeshi kutoka Uganda, Burundi na Kenya, tangu hapo
wamedhibiti sehemu kadhaa kutoka kwa wapiganaji hao.
Lakini mashambulizi ya kuvizia yanayofanywa na kundi hilo dhidi ya
maslahi ya majeshi ya serikali na yale ya kigeni, yameondoa matumaini ya
kunusuru taifa hilo kutokana na vita vya miaka mingi.
Chanzo: BBC Swahili
Chanzo: BBC Swahili