WATU wawili wamefariki
dunia hapo hapo na wengine nane kujeruhiwa baada ya gari aina ya Noah
walilokuwa wamepanda kutaka kulipita gari lililkuwa mbele yake na
kukutana na lori aina ya Volvo na kugongana uso kwa uso na kusababisha
vifo hivyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,Costastine Massawe athibitisha kutokea tukio hilo jana na kueleza tukio hilo lilitokea majira ya
saa tano adhuhuri wakati gari hilo aina ya Noah T266 AXZ
lililokuwa likitokea Kabuku kwenda Mkata ambapo lilipofika eneo la
Kwamgogo ndio lilipotaka kulipita gari lililokuwa mbele yake na ndipo
alipokutana na lori aina ya Volvo na kugongana nalo.
Massawe
ametaja dereva wa gari aina ya Noah aliyesababisha ajali hiyo kuwa ni
Abdallah Selehe (60) mkazi wa kata ya Hale wilayani Korogwe mkoani Tanga
ambaye alikimbizwa kwenye hospitali ya Mkata, Handeni akiwa hajitambui
akiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi.
Aliwataja watu
waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni wanawake wawili ambao
walikuwa miongoni mwa abiria waliokuwepo kwenye gari hilo aina ya Noah
ambapo aliwataja majina kuwa ni Mary Mushi (56) na Sikudhani Hussein
wote wakazi wa wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani.