Rais Obama amwalika Rais JK Kuhudhuria Mkutano Wa Wakuu Wa Nchi Za Afrika ....




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Marekani Mheshimiwa Barack Obama amemwalika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika ambao anauandaa katika mji mkuu wa Marekani, Washington baadaye mwaka huu.

Mkuu wa Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), Bwana Rajiv Shah amewasilisha mwaliko huo wa Rais Obama kwa Rais Kikwete wakati wa mkutano wao uliofanyika leo, Alhamisi, Januari 23, 2014, katika Ukumbi Mkuu wa Mikutano ya Taasisi ya Uchumi Duniani (WEF) Davos, Uswisi.

Bwana Shah amemwambia Rais Kikwete kuwa Rais Obama amemwalika Rais Kikwete kuwa miongoni mwa viongozi wa 
Afrika ambao watahudhuria Mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika na Rais Obama uliopangwa kufanyika Agosti 5-6 mwaka huu mjini Washington.

Bwana Shah amemwomba Rais Kikwete kusaidia kutoa mchango wa mawazo kuhusu jinsi gani ya kufanikisha mkutano huo ambao unazungumzia jinsi Marekani inavyoweza kuongeza kasi ya kusambaza umeme katika Afrika chini ya Mpango wa Marekani wa Power Africa.

Aidha, Bwana Shah amemwomba Rais Kikwete kusaidia mawazo yake ya jinsi ya kusaidia ajenda ya pili ya kikao hicho ambayo ni jinsi ya kuongeza mafanikio ya Mpango wa Kuboresha Kilimo katika Afrika wa Grow Africa ambao unaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na Marekani.

Hii ni mara ya tatu kwa Rais Obama kumwalika Rais Kikwete kushiriki katika shughuli za kiongozi huyo wa Marekani na za Serikali yake. Miezi mitatu tu baada ya kushika madaraka mwaka 2008, Rais Obama alimwalika Rais Kikwete kuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika kutembelea Ikulu ya Rais Obama na kufanya mazungumzo naye.

Ilikuwa kwenye mkutano wao ambako Rais Obama alimwuliza Rais Kikwete nini utawala wake Rais Obama ungeweza kulifanyia Bara la Afrika na Rais Kikwete akamwambia Rais Obama kuwa njia rahisi zaidi ya kusaidia Bara la Afrika ni kusaidia kuendeleza kilimo kwenye bara hilo ambako mamilioni kwa mamilioni ya watu wanategemea kilimo kwa maisha yao. Rais Obama aliukubali ushauri huo ambao anautekeleza kwa njia nyingi kwa sasa.

Rais Obama pia alimwalika Rais Kikwete kuwa miongoni mwa viongozi watatu wa Afrika kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Tajiri na Zenye Viwanda Vingi Zaidi wa G-8 uliofanyika Camp David, Maryland, eneo la mapumziko ya mwishoni mwa wiki la viongozi wa Marekani.

Rais Kikwete amekubali mwaliko huo wa sasa akisema kuwa atawasilisha mapendekezo yake ya jinsi ya kufanikisha mkutano huo muda siyo mrefu kuanzia sasa.

Bwana Shah amemwambia Rais Kikwete kuwa mawazo yake yatasaidia kuongeza kasi ya jitihada za Marekani na nchi za Afrika katika kusambaza umeme na kuboresha kilimo kwenye Bara hilo.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

0 comments: