Mgogoro ndani ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo , umeingia katika sura mpya baada
ya viongozi wake wawili waandamizi, Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na
Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo kuuandikia uongozi wa chama hicho
wakitaka uikane taarifa inayowachafua mitandaoni.
Zitto na Dk Mkumbo wanatuhumiwa kupokea
fedha na kushirikiana na viongozi wa Idara ya Usalama wa Taifa na wale
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nia ya kuivuruga Chadema.
Taarifa hiyo yenye kichwa cha habari
`Ripoti ya siri juu ya Zitto Kabwe’, ambayo imesambaa katika mitandao
mbalimbali ya kijamii katika siku za karibuni inadaiwa kuwa iliandaliwa
na Kitengo cha Upelelezi cha Chadema baada ya uchunguzi wa mwenendo wa
Zitto ndani na nje ya nchi kuanzia mwaka 2008.
Sehemu ya taarifa hiyo ya mtandaoni
inadai kuwa Zitto alipelekewa kiasi cha Dola za Marekani 266,000 (Sh416
milioni) huko Ujerumani na maofisa wa Usalama wa Tanzania, Desemba 16,
2009.
Ripoti hiyo inadai kuwa fedha hizo
zilipitishwa katika Benki ya Berliner ya Ujerumani kwenye akaunti ya
raia wa nchi hiyo, Andrea Cordes, ambaye anadaiwa kumpelelekea Zitto.
Taarifa zaidi zinadai kuwa fedha hizo ziligawiwa kwa wafuasi mbalimbali wa chama hicho na miongoni mwao ni Dk Mkumbo.
Zitto amlima barua Dk Slaa
Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari jana, Zitto alisema amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willbrod Slaa kumwomba athibitishe ‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ kama ni
ya kweli au chama hicho kiikanushe ili aweze kuchukua hatua za kisheria
dhidi ya waandishi wa kile alichokiita ‘hekaya.’
“Taarifa ya Chadema inasema kwamba chama
hicho (chama changu), kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka
2008 hadi 2010 na kubaini kuwa mimi ninapokea fedha kutoka Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema,” alisema Zitto kwenye taarifa
yake.
Zitto alisema taarifa hiyo ni ya kutunga
na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imemfedhehesha, imemsikitisha
na kumkasirisha.
Alisema taarifa hiyo iliibuliwa katika
kipindi ambacho alikuwa ziarani barani Ulaya katika nchi za Uswisi na
Uingereza ambako alikuwa anafuatilia fedha zilizofichwa na Watanzania
katika nchi hizo.
“Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa
ni kutaka kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya
kutaka Watanzania wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti
hiyo waliamua kutoa taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu,”
alieleza Zitto katika taarifa yake.
Dk Mkumbo alia na uenezi
Dk Mkumbo alieleza kusikitishwa na Idara ya Uenezi ya Chadema kwa kukaa kimya bila kutoa maelezo juu ya suala hilo.
“Hasa pale ambapo tumeambiwa waraka huu
umetoka makao makuu. Hii si kawaida kwa idara yetu hii nyeti
iliyosheheni watu mahiri. Mara zote huwa wepesi kabisa kwa vijana wetu
katika idara hii kutoa ufafanuzi, tena kwa mambo mepesi kabisa
yanayokigusa chama, vipi makamanda kwenye jambo hili imekuwaje?”
aliandika Dk Mkumbo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Facebook jana na
kuthibitisha kwa simu.
Dk Kitila alisema pamoja na umaskini wake, hajawahi kuhongwa popote na wala hatarajii.
“Taarifa zinazosambazwa kuhusu mimi ni
za uongo wa kijinga na uzushi wa kitoto kwa malengo ya siasa nyepesi. Ni
wazi kwamba wanaosambaza habari chafu kunihusu hawanijui na ndiyo maana
wanaweza kudiriki kuzusha kwamba mimi Kitila Mkumbo naweza kuhongwa
Sh200,000.”
Alihoji pia Chadema ilikuwa na siri gani
za hatari kiasi cha kumfanya Zitto, ambaye ni rafiki yake wa siku
nyingi kuhongwa kiasi hicho kikubwa cha fedha.
Mnyika awajibu
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa Chadema, John Mnyika ameikana ripoti hiyo na kueleza kuwa haijaandikwa na makao makuu ya Chadema.
Mnyika alisema Zitto ameibua kitu ambacho anafahamu kuwa kimeshughulikiwa na uongozi wa chama hicho.
“Zitto anajua kuwa Andrea Cordes
aliniandikia baruapepe na nakala kwake nikawajibu kuwa ripoti hiyo
haijaandikwa na makao makuu ya chama na tukipokea malalamiko rasmi
tutachunguza kwa sasa chama kinaichukulia ripoti hiyo kama ripoti
nyingine zinazosambazwa mitandaoni,” alifafanua Mnyika.
Akizungumzia malalamiko ya Dk Mkumbo,
Mnyika alisema alikuwa anapaswa kufuata taratibu za chama kama alikuwa
na malalamiko.Idara ingetoa ufafanuzi zaidi. Mjadala huu usikuzwe bila
sababu za msingi na kufunika masuala mengine muhimu ya kitaifa,” alisema
Mnyika.
Alisema baada ya taarifa hiyo ya siri
kusambaa mtandaoni, Zitto alitoa kauli na kama Dk Mkumbo hakuridhika,
alipaswa kuonana na watu wa Idara ya Uenezi ya Chadema.