Msemaji wa Tume hiyo, Omega Ngole alisema baada ya mwili huo kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam utapelekwa kuhifadhiwa Hospitali ya Lugalo.
Ratiba inaonyesha kuwa kesho saa 4.00 asubuhi kutakuwa na ibada ya kumwombea itakayofanyika kwenye Kanisa Katoliki la St Joseph, Dar es Salaam.
Baada ya kumalizika kwa ibada hiyo, mwili utapelekwa kwenye Viwanja vya Karimjee kwa ajili ya kuagwa kitaifa kuanzia saa 6.30 mchana na kisha utapelekwa nyumbani kwake Kibamba-Msakuzi.
Keshokutwa Jumapili kutakuwa na ibada fupi nyumbani kwake na baada ya hapo, safari ya kuelekea kijijini kwake, Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga, Kilimanjaro tayari kwa mazishi yaliyopangwa kufanyika keshokutwa.
Dk Mvungi alifariki dunia, Jumanne iliyopita kwenye Hospitali ya Millpark Johannesburg, Afrika Kusini baada ya kuumizwa na watu wasiojulikana waliomvamia nyumbani kwake, Novemba 3 mwaka huu.
Aacha kitabu
Katika hatua nyingine, Dk Mvungi aliwahi kuandika kitabu kiitwacho ‘Constitutional Reforms For Democratisation in Tanzania’ mwaka 1992 ambacho asilimia kubwa ya mapendekezo yake ndiyo yanayotumika katika mchakato wa sasa wa Katiba Mpya.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Kibamba-Msakuzi jana, Mkuu wa Shule ya Sheria katika Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Bonaventure Rutinwa alisema kitabu hicho ambacho kilitokana na mijadala mbalimbali kuhusiana na katiba, kinatumiwa pia na wanafunzi wa sheria.
“Yote ambayo unayaona sasa yakiwamo masuala ya mabaraza ya katiba, madaraka ya rais, tume huru ya kukusanya maoni, Bunge la Katiba na mambo mengine yapo katika kitabu hicho,” alisema Profesa Rutinwa na kuongeza kuwa hata kuchaguliwa kwake katika tume hiyo hakukuwa jambo la bahati mbaya.
Alisema Dk Mvungi hakwenda katika tume kwa kuvutiwa na malipo au posho bali, uzalendo wake.
“Rais Jakaya Kikwete alijua anamteua mtu wa namna gani na kikubwa zaidi mapendekezo yaliyomo katika kitabu hicho hata yeye Rais Kikwete anayajua,” alisema na kuongeza:
“Kwa kuandika kitabu cha namna hiyo wakati wa mfumo wa chama kimoja ulikuwa ujasiri usio wa kawaida”.
-Mwananchi