HADI anakata roho Novemba
12, mwaka huu, Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu wa
NCCR-Mageuzi, Dk. Sengondo Mvungi amepitia mateso makubwa.
Dk. Mvungi ambaye pia
alikuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Novemba 3, mwaka huu
alijeruhiwa kwa kukatwa na mapanga kichwani nyumbani kwake
Kibamba-Msakuzi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kulazwa kwenye
Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (Moi).
Tangu lilipotokea tukio
hilo, Dk.Mvungi aliishi katika mateso makubwa kutokana na kupoteza
fahamu huku akipumua kwa kutumia mipira ya gesi hadi kifo kilipomfika
katika Hospitali ya Milpark, Johannesburg, Afrika Kusini.
Kwa takribani siku tisa,
Dk. Mvungi alikuwa akisikilizia maumivu makali ya majeraha makubwa ya
mapanga hivyo ni dhahiri kuwa alipitia mateso makubwa.
Watu kumi akiwemo John
Mayunga ambaye ni mtuhumiwa wanaodaiwa kuvamia nyumbani kwa Dk. Mvungi
wanashikiliwa na jeshi la polisi jijini Dar kwa ajili ya mahojiano zaidi
juu ya tukio hilo.
Watu hao walikamatwa wakiwa na mapanga pamoja na simu ya marehemu.