RAISI KIKWETE ATUA SRI LANKA KUHUDHURIA MKUTANO WA JUMUIYA YA MADOLA

Rais Jakaya Kikwete, amewasili kwenye mji wa Colombo, Sri Lanka, tayari kwa mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, unaoanza leo.
 
Rais Kikwete aliyefuatana na mkewe Mama Salma Kikwete, anahudhuria mkutano huo wa siku tatu utakaofanyika kwenye eneo la Nelum Pokuna mjini Colombo.
Mkutano huo utafunguliwa rasmi na Prince Charles, ambaye ni mtoto wa Malkia wa Uingereza na atafanya hivyo kwa niaba ya mama yake, Malkia Elizabeth.
Malkia huyo ndiye kiongozi wa Jumuiya ya Madola, ambaye hata hivyo, hataweza kuhudhuria mkutano wa mwaka huu.
Mara baada sherehe za ufunguzi, Rais Kikwete ataungana na viongozi wenzake kwa ajili ya vikao rasmi vya mkutano huo vitakavyofanyika katika Kituo cha Maonyesho ya Kumbukumbu cha Sirimavo Bandaranaike.
Miongoni mwa shughuli kubwa za leo ni pamoja na vikao viwili vya kwanza vya viongozi wa jumuiya hiyo na baadaye majadiliano.
Viongozi hao pia watahudhuria hafla rasmi ya makaribisho itakayoandaliwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Kamalesh Sharma katika Ukumbi wa Bandaranaike.
Jana Rais Kikwete na ujumbe wake, walihudhuria hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na Prince Charles na mkewe.
Jumuiya ya Madola inahusisha nchi zilizokuwa chini ya ukoloni wa Uingereza na nyingine ambazo zenyewe ziliomba na kukubaliwa kujiunga nayo. Nchi hizo ni pamoja na Msumbiji na Rwanda.