HII NDO SIRI ZA KUDUMISHA PENZI LISITETEREKE...!!

UNAWEZA kuanzisha kitu chochote, wakati wowote lakini jambo la msingi zaidi ni namna ya kudumisha na kuendeleza ulichokianzisha. Kwa mfano, unaweza kufungua biashara fulani lakini ukafeli katika kuisimamia na kufuja fedha, hutafanikiwa!

Marafiki zangu, ndivyo ilivyo hata kwenye uhusiano. Unaanzisha sawa, lakini vipi kuhusu kudumisha penzi lako likaendelea kuwa na nguvu zaidi siku hadi siku? Hilo ndilo somo tunaloendelea kulijadili hapa kwenye Let’s Talk About Love.

Kama mtakumbuka vizuri, wiki iliyopita nilianza kwa kufafanua namna ya kutambua thamani na kuithamini. Bila kujua thamani yako wewe kwanza, kujithamini na kumuona mwenzi wako ni wa muhimu kwako, hutaweza kudumisha penzi lako.
Hebu sasa tuendelee kujifunza katika vipengele vingine marafiki zangu.

MHESHIMU
Mwanaume anapenda sana kuheshimiwa na mpenzi wake. Kwa kawaida, mwanaume akigundua haheshimiwi au unafanya hivyo kwa kumridhisha tu na si kutoka moyoni, ni rahisi kukuacha.
Kama kichwa cha familia, lazima apewe nafasi ya kutoa uamuzi tangu mapema. Ikiwa utakuwa na majibu mabaya kwake, huonyeshi heshima ni wazi kwamba atakuacha mapema, maana utakuwa umepoteza sifa za kuwa mama wa familia.

KUWA MFARIJI WAKE
Siku hazifanani, hivyo inawezekana kabisa siku moja mwenzi akawa na matatizo aidha ya kiakili, kimaisha au kikazi. Ikitokea umegundua mpenzi wako ana matatizo na hana furaha, wewe ndiyo unatakiwa kuwa mfariji wake.
Lazima umsome, ujue yukoje ili iwe rahisi kugundua tofauti atakayokuwa nayo siku akiwa hayupo sawa. Kumfariji ni jukumu lako, utakuwa umeonesha uwezo wako kikamilifu wa kuwa mama bora hapo baadaye.

Mama ambaye anaweza kurudisha amani ya mume wake, pindi inapokuwa mashakani. Ni mambo yanayowezekana kabisa marafiki zangu. Lazima ujipe umuhimu kwa mwenzako. Akikaa afikirie na kuona kuwa kweli wewe ni muhimu katika maisha yake.

Aone kuna ulazima wa kuharakia ndoa mapema kwa sababu utakuwa umemjengea imani ya moja kwa moja. Huo ndiyo ukweli marafiki zangu. Ikiwa kinyume cha hapo, ni kwamba utakuwa unajiondoa mwenyewe kwenye sifa ya kuwa mke sahihi.

KAULI
Inakupasa uwe na ulimi mtamu. Simaanishi uuweke sukari ili uwe mtamu; hapa nazungumzia juu ya kauli njema. Hutakiwi kuwa na majibu ya hovyo kwa mwenzako, uzungumze kwa staha na heshima. Hapo utakuwa unaingia moja kwa moja kwenye nafasi ya kuwa mke.

Wale wa mitaani, wanasikiliza maneno ya hovyo kutoka kwa marafiki zao ndiyo wanaoweza kuwa na lugha chafu kwa wenzao. Kauli mbaya hukuondolea sifa ya ustaarabu na moja kwa moja unajiweka pembeni mwenyewe. Nani atapenda kuwa na mtu ambaye hajiheshimu? Ana majibu mabaya? Hajali kinachotoka kinywani mwake? Ni nani?

ACHANA NA MAKUNDI
Mwanamke mwenye staha hafungamani na makundi ya mashangingi wa mjini. Wanaume hasa wanaotaka kuoa, hawapendi mke mtarajiwa awe shangingi au anayejihusisha na wanawake wa aina hiyo.

Inaaminika kwamba kwenye makundi hayo hujadiliwa mambo yasiyofaa ndiyo maana wanaume wengi hawapendi wanawake wenye tabia za kukaa kwenye makundi ya mashangingi. Chukua hii kwa faida yako.

-GPL