MWENYEKITI wa CCM Kijiji cha Chole wilayani Kisarawe, Mkoani Pwani, Kondo Shamte yuko katika hali mbaya sana baada ya kuchomwa mkuki tumboni na wafugaji wa kabila la Wamang’ati na kusababisha utumbo wake kuwa nje.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo ambaye kwa nafasi yake kijijini hapo
ndiye anayeheshimika zaidi, tukio hilo lilijiri Agosti 28, mwaka huu.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa nyumbani kwake kijijini hapo,
Kondo alisema katika kijiji hicho kulijengwa barabara na wahisani
(hakuwataja jina). Wanakijiji wakaombwa kuitunza barabara hiyo kwa
masharti kwamba wasipitishe mifugo.
Alisema siku ya tukio, wafugaji hao walipitisha mifugo katika
barabara hiyo licha ya amri iliyokuwepo, alipoona hali hiyo aliwafuata
na kuwaomba wapitishe pembeni.
“Walikataa, nikaamua kuwatuma wajumbe wangu wawafuatilie kwa nyuma
ili wasiendelee kupitisha mifugo hiyo,” alisema mwenyekiti huyo.
Akaendelea: “Baada ya wafugaji hao kuona nimetuma wajumbe wakarudi
hadi nilipokuwa nimesimama na kuniambia kuwa niliwatuma wale wajumbe ili
wakawafanyie fujo, wakatoa vitisho kwamba ule ndiyo ungekuwa mwisho
wangu.
Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa kabla yeye
hajazungumza chochote, mfugaji mmoja alichomoa mshale na kumrushia
ambapo ulimwingia tumboni kisha wote wakakimbia.
Alisema alijitahidi sana kuutoa mshale huo huku tayari akiwa
ameanguka chini. Alipofanikiwa, ndugu na jamaa nao walitokea na
kumkimbiza Hospitali ya Kisarawe.
“Pale hospitalini Kisarawe ilishindikana kunitibu, nikakimbizwa
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Dar es Salaam) ambako nilifanyiwa
upasuaji mkubwa kwa kukata sehemu ya utumbo iliyoharibika,” alisema.
Mwenyekiti huyo aliendelea kuweka wazi kwamba baada ya operesheni
hiyo daktari alimwambia ni lazima sehemu ya utumbo utolewe nje mpaka
sehemu ya ndani ipone vizuri ndipo waurudishe, hivyo kwa sasa haja kubwa
anaitolea ubavuni.
“Hivi sasa haja kubwa natolewa kwa hapa ubavuni mpaka nitakaporudi tena hospitali mwezi Desemba, mwaka huu,” alisema.
Hata hivyo, Kondo alisema kitu kinachomuuma zaidi ni kutomuona kiongozi
wa CCM hata mmoja aliyefika nyumbani kwake kumjulia hali wala kumpa
msaada wowote kwani hivi sasa yuko katika hali ngumu ya kimaisha
kutokana na gharama za kutibu kidonda chake kuwa juu.