Mfanyabiashara
maarufu , Nickson Mushi, mkazi wa Msasani Maili sita mjini hapa,
ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi baada ya
kuvamia nyumbani kwake muda mfupi baada ya kurejea kutoka katika
shughuli zake.
Mushi ambaye ni mfanyabiashara wa Mbao aliuawa na watu wasiojulikana ambao wanaaminika walitumia silaha za moto kutekeleza uhalifu huo kisha kumkata katika maeneo ya mikono kwa kutumia panga.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, majambazi hayo baada ya kumuua
yalimpora kiasi kikubwa cha fedha zinachokadiriwa kuwa Sh. milioni 16 na
18 na simu mbili.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema tukio hilo lilitokea juzi usiku wakati mfanyabiashara huyo akiwa na mkewe wakitoka katika shughuli zao za kazi.
Alisema wakiwa njiani wakikaribia kufika nyumbani kwao,gari moja
dogo aina ya Saloon iliwapita na baadaye wakati wakikaribia getini
watu waliokuwa kwenye gari hilo walishuka na kisha kumpiga risasi na
kumpora fedha.
Kamanda
huyo alisema baada ya uchunguzi katika eneo la tukio kulikutwa risasi
tatu, maganda mawili ya risasi na bastola moja ambayo inadaiwa kuwa ni
mali ya marehemu.
Alisema polisi wameanza uchunguzi wa tukio hilo.