WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amekiri kwamba Serikali ilifanya uzembe katika kutatua taarifa za uchochezi zilizosababisha vurugu za Mtwara. Kauli hiyo aliitoa mjini Mtwara jana alipozungumza na wananchi wa Masasi akiwa njiani kuelekea wilayani Nanyumbu kufungua mradi wa umeme. Alisema baada ya kutokea kwa uzembe huo wako wajanja wachache waliotumia nafasi hiyo kufanikisha malengo yao.
“Katika hili tulizidiwa ujanja na watu wengine kwa kuwa walikuwa
wakiwaambia wananchi kwamba gesi itatolewa Mtwara na kupelekwa Dar es
Salaam.
“Tena wakasema ikishafikishwa Dar es Salaam ambako
vitajengwa vinu na gesi nyingine itapelekwa Bagamoyo kwao Rais Jakaya
Kikwete.
“Huo ulikuwa ni upotoshaji mkubwa tena mkubwa kweli
lakini sisi tulilichukulia juu juu, hatukutazama kwa undani kulieleza
hilo na wajanja wakalipata na kulipotosha hilo,” alisema Pinda.
Alisema gesi itazalishwa Mtwara ingawa vinu vitajengwa Dar es Salaam kwa ajili ya kuisambaza gesi hiyo kwa watumiaji wengine.
“Wakati
nazungumza na watu wa Mtwara mwaka jana, walinieleza mambo mengi sana
juu ya hiyo gesi na mwishowe nikawauliza hivi kwanini hamtaki gesi itoke
Mtwara.
“Nikawauliza, hivi ikija meli hapa Mtwara ikapaki pale
bandarini na kupakia gesi na kuipeleka Uarabuni mtakataa, wakasema
hatuna shida, nikawauliza tena je, meli hiyo hiyo ikipakia gesi na
kuipeleka Dar es Salaam, mna tatizo, wakasema hatuna tatizo.
“Sasa
nikawauliza tatizo lenu ni nini, wakasema ni hilo bomba lenu hilo
mnalojenga. Mimi nikawaambia gesi itazalishwa hapa Mtwara, tena katika
Kijiji cha Madimba na itakayopelekwa Dar es Salaam haitazidi asilimia
10.
“Nikawambia gesi ikianza kuzalishwa mtanufaika kwa kuwa hata
viwanda vitakuwapo kikiwamo cha Dangote kitakachozalisha saruji pale
Kijiji cha Msijute,” alisema Pinda.
Kuhusu hasara iliyopatikana
baada ya wananchi kufanya vurugu na kuharibu mali, alisema bado
inafanyiwa kazi na itakapokamilika italetwa mkoani Mtwara.
“Baada
ya vurugu zile, Serikali ilifanya tathimini ya matukio na ikiwezekana
kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha huu itakuwa imekamilika na tutaangalia
la kufanya ingawa nataka niwahakikishie kwamba jambo hili tunalifanyia
kazi na litakapokamilika tutalirudisha kwenu,” alisema Pinda.
Aliwashukuru
viongozi wa Mkoa wa Mtwara kwa kutochukua uamuzi wa kulipa kisasi
wakati wa vurugu hizo kwa kuwa kama wangeamua kufanya hivyo hali
ingekuwa mbaya zaidi.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Farida
Mgomi, alisema vurugu hizo zilizotokea Januari 26, 2013 zilisababisha
hasara ya Sh bil 3.4.
>>Mtanzania
>>Mtanzania
0 comments:
Post a Comment