Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) naSerikali yake kuacha kile alichokielezea kuwa ni hila ya kutaka kukwamisha mchakato wa Katiba Mpya.
Mchakato huo sasa unaelekea katika hatua ya Bunge
Maalumu la Katiba. Amesema Watanzania hawako tayari kurudi nyuma
kuendelea na katiba ya sasa.
Alikuwa akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara huko
Ngara, mkoani Kagera juzi, ambao ni sehemu ya operesheni ya Movement For
Change (M4C) iliyopewa jina la ‘Pamoja Daima’.
Mbowe alisema yupo tayari kuwa wa kwanza kufungwa
kwa kosa la kudai Katiba Mpya kama Serikali itaweka mazingira ya hila
ambayo yatalazimisha kukwamisha mchakato wa kupata Katiba Mpya na
kuwafanya Watanzania kuendelea na Katiba ya mwaka 1977.
Alisema watawala wasitumie hila na mwanya wowote
kuitia nchi majaribuni kwa kulazimisha watu kuishi na katiba iliyokosa
uhalali wa kisiasa na kisheria.
Alisema badala yake, wanatakiwa kuhakikisha kuwa kunakuwa na mazingira mazuri kwa Watanzania kujiamulia nama ya kuongozwa
Kiongozi huyo wa Chadema alisisitiza kuwa Katiba ni uhai wa taifa na si matakwa ya chama chochote cha siasa wala mtu binafsi.
Alisema Watanzania wengi wamependekeza kuwapo kwa
shirikisho la Serikali tatu katika Rasimu ya Katiba Mpya, lakini akadai
kuwa zipo njama zinazofanywa za kuchakachua uamuzi huo wa wananchi kwa
ajili ya kukilinda CCM. Alisema kama hila hizo za kupindua maoni ya
wananchi zitafanikiwa kupenyezwa kupitia bungeni, yuko tayari kuungana
na Mtanzania yeyote kuzunguka nchi nzima kuwahamasisha wananchi waikatae
rasimu hiyo.
Alisisitiza kwamba endapo wananchi wataikataa
Katiba hiyo, pia hawatakuwa tayari kurudi kuendelea kutumia katiba ya
zamani inayotumika hivi sasa kama ambavyo Serikali imekwishasema.
“Watawala lazima wajue. Watanzania hawa ambao
wameipigania na kuililia Katiba Mpya kwa muda mrefu sasa hawako tayari
tena kurudi nyuma,” alisema kiongozi huyo wa Chadema
-mwananchi
-mwananchi
0 comments:
Post a Comment