Polisi katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wanawashikilia watu
watatu kwa tuhuma za kumpiga na kumjeruhi Mwenyekiti wa Chadema wilayani
Temeke, Joseph Yona, ambaye baadaye, alitelekezwa Ununio, Kunduchi.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea mapema wiki hii.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema kwa sasa watu hao wanahojiwa kabla ya kuwafikisha mahakamani.
Alisema watuhumiwa, walikamatwa kwa nyakati tofauti juzi na jana. “Tunawahoji na uchunguzi ukikamilika tutawafikisha mahakamani,” alisema Kova.Kamanda huyo alisema polisi pia wanaendelea kuwatafuta wahusika wengine wa tukio hilo.
Baada ya kujeruhiwa, Yona alifikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako katika simulizi zake alisema alitekwa akiwa Mtoni kwa Aziz Ali.
Alisema alitekwa saa 5:00 za usiku na kuingizwa katika gari moja kwa maelezo kuwa alikuwa anapelekwa polisi lakini njiani alipigwa na kwenda kutelekezwa Ununio.
Alisema kabla ya kutekwa, alikuwa ameketi na vijana wanne wa Tawi la Chadema la Ukombozi na kwamba ghafla walijitokeza watu kama sita ambao walimnyanyua kwa madai kuwa alikuwa anatakiwa polisi.
CHANZO; MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment