Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na
Maji (EWURA), katika kikao chake cha tarehe 10 Desemba 2013 pamoja na
mambo mengine, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme kwa viwango
mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja hatua ambayo itaongeza mzigo
wa gharama za maisha kwa wananchi na itaathiri uchumi wa nchi.
Maamuzi hayo yamefikiwa kufuatia tarehe 11 Oktoba 2013, Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO) kuwasilisha maombi ya kurekebisha bei ya umeme
kwa EWURA. TANESCO ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia 67.87 kuanzia
tarehe 1 Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1 Januari 2014 na
asilimia 9.17 kuanzia tarehe 1 Januari 2015.
Vilevile TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei
ya umeme kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na
mabadiliko ya thamani ya shilingi ya kitanzania.
Maamuzi hayo ya Bodi ya EWURA ambacho ni chombo cha Serikali
yamethibitisha kwamba Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo
alisema uongo kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 na 2013
alipowahakikishia wananchi kwamba bei ya umeme haitapanda hata baada ya
TANESCO kuwasilisha mapendekezo ya kupandisha bei ya umeme.
Aidha, kwa kuwa leo tarehe 9 Januari 2014 Waziri Muhongo amenukuliwa
na baadhi ya vyombo vya habari akisema kwamba sekta ya nishati sio
porojo; natoa mwito kwake kuanza kwanza kujirekebisha yeye mwenyewe kwa
kuacha porojo na uongo na kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuzuia
utekelezaji wa maamuzi ya kupandisha bei ya umeme ambayo yataongeza
ugumu wa maisha kwa wananchi kinyume na ahadi ya maisha bora kwa kila
mtanzania iliyotolewa na CCM.
Pia, kwa nafasi ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini natoa mwito kwa
wote wenye kuathirika na maamuzi hayo ndani ya wiki moja kuanzia sasa
watume maoni na mapendekezo yao kwa barua pepe kupitia anuani
mbungeubungo@gmail.com.
Maoni na mapendekezo hayo yanaweza pia kutumwa kwa njia nyingine za
kuwasiliana na Ofisi ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Maoni na mapendekezo
hayo yahusu athari ambazo wamezipata na/au wanatarajia kuzipata kutokana
na maamuzi hayo na mapendekezo ya hatua ambazo wanataka zichukuliwe.
Narajia kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wananchi mbalimbali
hususan kutoka pia kwa wateja wa TANESCO ambao wamepandishiwa bei katika
makundi yafuatayo:
Kundi D1: Hili ni kundi la wateja wadogo wa majumbani, hasa vijijini,
ambao hutumia wastani usiozidi wa Uniti 75 kwa mwezi. EWURA imeongeza
wigo wa mahitaji ya umeme na kufikia uniti 75 kwa mwezi, kwa kile
kilichoelezwa kuwa lengo likiwa ni kuongeza idadi ya wateja wa TANESCO
wanaoweza kulipa kidogo kwa matumizi ya umeme kwa kiwango hicho, na pia
kuwahamasisha kutumia zaidi umeme.
Awali kundi hili lilikuwa linatunia wastani wa matumizi ya uniti 50 kwa mwezi. Bei mpya ni shilingi 100 kwa uniti moja, kutoka shilingi 60 za sasa, sawa na ongezeko la shilingi 40.
Awali kundi hili lilikuwa linatunia wastani wa matumizi ya uniti 50 kwa mwezi. Bei mpya ni shilingi 100 kwa uniti moja, kutoka shilingi 60 za sasa, sawa na ongezeko la shilingi 40.
Kundi T1: Hili ni kundi la watumiaji wakubwa wa umeme majumbani,
biashara ndogondogo, mashine za kukoboa na kusaga nafaka, taa za
barabarani, mabango n.k. Bei iliyoidhinishwa ni shilingi 306 kwa uniti
moja, ikiwa ni ongezeko la Shilingi 85 ya bei ya sasa. TANESCO
ilipendekeza ongezeko la shilingi 131.
Kundi T2: Hili ni kundi la watumiaji umeme wa kawaida ambao hupimwa
katika msongo wa volti 400, na ambao matumizi yao ya wastani kwa mwezi
ni zaidi ya uniti 7,500 wateja wafanyabiashara kubwa, viwanda vya kati.
Bei ya nishati iliyoridhiwa ni shilingi 205 kwa uniti moja, sawa na
ongezeko la shilingi 73 ya bei ya sasa. TANESCO walipendekeza ongezeko
la shilingi 145 ya bei ya sasa.
Kundi T3-MV: Hili ni kundi la wateja wakubwa kama viwanda vikubwa
waliounganishwa katika msongo wa kati (Medium Voltage). EWURA
imeidhinisha bei ya nishati kwa kiwango cha shilingi 166 kwa uniti moja,
sawa na ongezeko la shilingi 45 ya bei ya sasa. TANESCO walipendekeza
ongezeko la shilingi 148 kwa uniti moja.
Kundi T3-HV: Hili ni kundi la wateja wakubwa waliounganishwa katika
msongo wa juu (High Voltage – Voti 66,000 na zaidi) ikiwa ni pamoja na
ZECO, Bulyanhulu, na Twiga Cement. Bei iliyoidhinishwa ni shilingi 159
kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 53 la bei ya sasa. TANESCO
waliomba ongezeko la shilingi 80 kwa uniti moja.
Mara baada ya kupokea maoni na mapendekezo hayo, pamoja na hatua
ambazo nitachukua kupitia nafasi ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
nitawasilisha pia mapendekezo kwa Kambi Rasmi ya Upinzani kuchukua hatua
za kibunge na CHADEMA kuchukua hatua za nje ya Bunge ili kunusuru
uchumi wa nchi na kutetea maslahi ya wananchi.
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini 09/01/2014
CHANZO; GPL
0 comments:
Post a Comment