Uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kuwaacha katika Baraza la
Mawaziri, mawaziri wote waliotajwa na CCM kuwa wameshindwa kutekeleza
majukumu yao umekichanganya chama hicho, baada ya jana kusema kuwa
hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mawaziri hao na wengine, iwapo
watashindwa kurekebisha upungufu wa kiutendaji unaozikabili wizara zao.
Chama hicho kilitoa ufafanuzi huo jana ikiwa
zimepita siku tano tangu Rais Kikwete alipofanya mabadiliko katika
baraza hilo na kuwaacha mawaziri saba waliohojiwa na CCM wakidaiwa ni
‘mzigo’, baada ya utendaji wao wa kazi kulalamikiwa na wananchi pamoja
na wabunge.
Desemba 14 mwaka jana CCM kupitia kikao chake cha
Kamati Kuu iliwahoji mawaziri hao, kisha ikamtupia mpira Rais Kikwete
kuamua hatima yao, huku kikifafanua kuwa “kilimshauri mambo matatu; ama
kuwafukuza, kuwahamisha wizara au kuwahimiza wafanye kazi.”
Uamuzi huo ulikuja baada ya chama hicho kufanya
ziara ya siku 26 iliyokuwa ikiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho,
Abdulrahman Kinana, mwishoni mwa mwaka jana katika mikoa ya Ruvuma,
Mbeya na Njombe na kukumbana na malalamiko ya wananchi kuhusu utendaji
kazi mbovu wa wizara zinazosimamiwa na mawaziri hao.
Mawaziri walihojiwa na CCM na wamebakizwa katika
Baraza la Mawaziri ni Dk Shukuru Kawambwa (Elimu), Christopher Chiza
(Kilimo), Saada Mkuya (Fedha). Mkuya alihojiwa kwa niaba ya aliyekuwa
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa ambaye kwa sasa ni marehemu). Wengine
ni Dk Abdallah Kigoda (Viwanda), Dk Mathayo David (Mifugo na Uvuvi),
Celina Kombani (Utumishi wa Umma) na Hawa Ghasia (Tamisemi).
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema;
“CCM hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya
mawaziri na watendaji wengine watakaoshindwa kurekebisha upungufu
unaopigiwa kelele. Kushindwa kwao kutimiza majukumu yao ni hujuma kwa
Ilani ya Uchaguzi ya CCM, hivyo chama hakiwezi kuvumilia usaliti huo.”
Alisema CCM kuendelea kuwafumbia macho watu
wasiopenda kuwajibika ni sawa na kujinyonga chenyewe, kusisitiza kuwa
chama kitaendelea na utaratibu wa kuwahoji watendaji wa Serikali na
wasiotaka kuhojiwa wajiondoe serikalini au watafute kazi nyingine za
kufanya. “Wanalipwa mshahara kwa kodi za Watanzania lazima wakubali
kuhojiwa, CCM katika hili tutakuwa wakali zaidi. Tunaungana na wabunge
wa CCM na wananchi kuhusu maoni ya utendaji kazi wa mawaziri hao,
malalamiko yao ndiyo yalizaa neno mawaziri ‘mzigo” alisema.
Nape alisema chama hicho kitatumia wingi wa
wabunge na madiwani wake kuisimamia Serikali na usimamizi huo kuanzia
sasa utaimarishwa zaidi katika ngazi zote, “Tutaisifu Serikali ikifanya
vizuri na tutaikosoa na kuishutumu ikifanya vibaya.
“Uwajibikaji wa kweli ndiyo msingi wa mafanikio na
maendeleo ya nchi yetu. Tuna matumaini mawaziri hawatayaangusha
matumaini ya wananchi kwa Serikali yao. Kuteuliwa kwao upya au kuachwa
kwenye Baraza la Mawaziri hakufuti upungufu wao uliotokea siku za
nyuma.”
Alisema ziara za chama hicho pamoja na utaratibu
wa kuwahoji watendaji wa Serikali umekuwa na mafanikio makubwa. Sasa
urasimu uliokuwapo awali katika ununuzi wa pamba, korosho, msongamano wa
magari katika mpaka wa Tanzania na Zambia (Tunduma) na upatikanaji wa
mbolea umemalizika. “Tunaongeza ukali maana muda wa kutekeleza Ilani ya
Uchaguzi ya chama ni mdogo, tukicheka na wasiopenda kuwajibika wananchi
watatuadhibu. Hatuko tayari kuadhibiwa kwani tumetoa ahadi kwa
Watanzania ni lazima tuzitekeleze,” alisema Nape.
Huku akiwataka Watanzania wawape muda mawaziri
hao, Nape alisisitiza: “Kama mambo yasipoenda wananchi waseme na CCM
itaungana nao kupiga kelele na kuhakikisha hatua zinachukuliwa. Ndiyo
maana hata wakuu wa mikoa na wilaya nao wanahojiwa na kutoa ufafanuzi
katika masuala mbalimbali.”
Alipoulizwa kama CCM itaendelea kuwavumilia Dk Kawambwa na
Chiza, Nape alisema, “Wamerudishwa, ila tunatumaini upungufu wameuona,
wakishindwa CCM haitakaa kimya. Ila wananchi wanatakiwa kutambua kuwa
kumfukuza waziri siyo suluhisho.”
Akitoa mfano, Nape alisema CCM haiwezi kuendelea
kuvumilia kuona vinachapishwa vitabu vya shule za msingi na Sekondari
vyenye makosa.
“Mabwana shamba wiki nzima wanavaa suti badala ya
kwenda shambani. Angalia bosi wao anafanyaje (Chiza). Haiwezekani kwa
muda wa miaka minne na nusu Waziri Chiza hajakwenda kutembelea ghala la
taifa la chakula lililopo mkoani Ruvuma, nasema hivi, ukitaka
usinyooshewe kidole kaa nyumbani kwako.”
Vilevile alizungumzia jinsi mawaziri wanavyofanya
sherehe baada ya kuteuliwa, “Watu wanadhani kuteuliwa ni ulaji, vijana
wa nchi hii wabebe vita hii. Hivi sasa tukihesabu safari za mawaziri
kwenda nje ya nchi na kuwatembelea wananchi, zipi zitakuwa nyingi?”
alihoji.
Kuhusu madeni ya walimu, alieleza kushangaa kwa
nini yanaongezeka kila mwaka na kuhoji iweje Serikali imefikia hatua ya
kuwakopa wananchi badala la wananchi kuikopa Serikali.” Nape aliponda
utaratibu wa watendaji wa Serikali kufanya vikao kila siku na kushindwa
kuwahudumia wananchi, huku akisisitiza kuwa azimio la Sekretarieti ya
CCM ni kuhakikisha kuwa chama hicho kinakuwa karibu na wananchi,
kusikiliza changamoto zao na kuwasemea wanyonge.
0 comments:
Post a Comment