Mwezi mmoja tangu atambulishe toleo jipya la mavazi ‘Supremacy’
mbunifu wa mitindo nchini Martin Kadinda yuko mbioni kuanza ziara
aliyoipa jina la Boda to Boda, kutambulisha toleo hilo kimataifa.
Akizungumza na Mwananchi jana, Kadinda aliyetamba
miaka miwili nyuma na toleo la ‘six button’, alisema ziara hiyo itaitwa
Boda to Boda, na mpaka sasa ameshapata mwaliko katika nchi mbili ambazo
ataenda kutambulisha toleo hilo wiki chache zijazo.
“Boda to Boda ni programu nitakayozunguka nayo
nchi mbalimbali kwa ajili ya kuonyesha kazi zangu mpya zitakazotambulika
kama ‘supremacy.’ Mpaka sasa nimeshapata mwaliko kutoka nchi ya Kenya
na Zambia. Hii imekuja baada ya vazi langu la ‘six button’ kufanya
vizuri ndani na nje ya nchi,” alisema Kadinda.
Hata hivyo Kadinda ziara zake pia itategemea na mwaliko katika nchi husika kwani hatoweza kutembelea kila nchi.
“Nina mikakati ya kufika Bara la Ulaya na Marekani lakini itategemea mwaliko kwani siwezi kuifanya programu hii bila wenyeji.”
Alisema toleo hilo jipya litakuwa maalumu kwa
wanaume pekee ambapo kutakuwa na aina tofauti za mavazi yaliyojulikana
kwa jina hilo.
“Ndani ya ‘Supremacy’ utakutana na ‘Kwachukwachu
Shirt’, triples na dry show haya ni mashati yenye rangi mbalimbali za
kupendeza lakini yatakayokuwa yakiutambulisha Uafrika zaidi, lakini pia
na nguo za aina nyingine. Nimeonelea kutengeneza mavazi ya wanaume
pekee, kutokana na ukweli kwamba hawa hawana mitindo mingi kama ilivyo
kwa wanawake, hata hivyo yatawahusu wanaume wajanja, kwani yanakwenda na
wakati,” alisema Kadinda.
Alisema toleo hilo, litajumuisha nguo mbalimbali za kiume zenye umaridadi kuanzia rangi, mpaka aina ya ushonaji wake.
“Nguo zinazotengenezwa na Martin Kadinda
zitazingatia ubora kuanzia kwenye rangi mpaka aina ya ushonaji wake
kwani hazitafanana na toleo lolote lile lililowahi kutengenezwa na
wabunifu wa ndani na nje ya nchi. Itakuwa ya kipekee kama ilivyokuwa
‘six button’,” alisema Kadinda.
Alisema katika soko lake kwa mwaka huu, amewalenga
Watanzania wa kawaida. “Hili ni soko kwa ajili ya Watanzania wa kawaida
sana, nimeanza kusambaza mzigo hapa nchini na sasa ninaanza kuitangaza
kimataifa.”
0 comments:
Post a Comment