Umechangia historia ya nchi yetu, Rais Kikwete amsifu Mzee Mkapa
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amemsifu na kumpongeza Rais wa tatu wa Tanzania, Mzee Benjamin William
Mkapa kwa kuchangia historia ya Tanzania kupitia uamuzi wake wa
kuchapisha vitabu vya hotuba zake alizozitoa wakati wa uongozi wake wa
miaka 10.
Rais Kikwete amemwambia Rais Mstaafu Mzee Mkapa: “
Pongezi sana Mzee Mkapa kwa uamuzi wako wa kuchapisha hotuba hizi.
Umefanya jambo kubwa. Umefanya jambo la maana. Umechangia historia ya
nchi yetu kwa kipindi chako cha uongozi kwa kuchapisha hotuba za kipindi
hicho cha uongozi wako.”
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Jumatano, Januari 15, 2014, wakati alipopokea nakala za vitabu vya hotuba za miaka 10 ya uongozi wa Rais Mkapa kutoka kwa Mzee Mkapa mwenyewe katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam.
Ameongeza Rais Kikwete: “Hotuba za Rais siyo za Rais wala mali yake. Ni historia ya nchi na lazima turekodi na kuweka kumbukumbu ya sehemu hii ya historia ya nchi yetu. Hotuba hizo zitaendelea kuvionyesha vizazi vijavyo mambo yaliyotokea wakati wa Urais wako, msimamo wako na wa nchi katika kipindi hicho na hata fikra zako zilizosaidia kusukuma mbele maendeleo ya nchi yetu.”
Rais Kikwete pia amemsihi Mzee Mkapa kuangalia namna ya kuweka historia ya uongozi wake katika kitabu kwa kadri alivyoshuhudia historia wakati wa miaka 10 ya uongozi wa Tanzania. “ Bado tunaendelea kusubiri kitabu chako Mzee.”
Rais Kikwete pia amesema kuwa ipo haja kwa wadau mbali mbali wa elimu, hasa wale wenye mapenzi ya kusoma vitabu, kuchukua hatua za kuamsha ari na mapenzi ya Watanzania kusoma vitabu ambayo kwa sasa amesema yamepungua sana. “Tuone namna ya kuamsha ari ya watu kupenda na kusoma vitabu.”
Akizungumza kabla ya kukabidhi vitatu hivyo na vilivyochapishwa kwa mvuto mkubwa, Mzee Mkapa amesema: “Kwa kweli hiki ni kitabu kimoja chenye machapisho matatu. Nimeamua kuchapisha hotuba zangu kuonyesha kuwa pamoja na kwamba nilikuwa Rais wa miaka 10 lakini kila siku ya uongozi wangu ilikuwa tofauti na mwezi mmoja wa uongozi ulikuwa tofauti na mwingine na hivyo matukio na hotuba zilikuwa tofauti.”
“Nimeamua vile vile kuwa nikupe wewe Mheshimiwa Rais heshima ya kwanza ya kupokea toleo la hotuba hizo kwa kukubadhi wewe nakala ya kwanza”.
Miongoni mwa watu wengine, sherehe hizo zimehudhuriwa na Wakurugenzi wa Kampuni ya Uchapishaji ya Mkuki na Ngao ya hapa nchini, ambayo ndiyo imechapisha vitabu hivyo, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Mzee Walter Bgoya.
Mwingine aliyehudhuria sherehe hizo ni Balozi Ombeni Y. Sefue, Mhariri wa hotuba hizo ambaye kwa miaka mingi alikuwa msaidizi wa Mzee Mkapa, Ikulu. Balozi Sefue sasa ni Katibu Mkuu Kiongozi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM. 15 Januari, 2014
0 comments:
Post a Comment