Joto la uteuzi wa Baraza la Mawaziri limeendelea kupanda hadi kufikia baadhi ya watu kuunda na kutangaza baraza ‘feki’ lililoibua mtafaruku kwenye jamii, kiasi cha kuwafanya wananchi kupiga simu chumba cha habari kutaka kujua ukweli wa taarifa hizo.
Hii
ni kufuatia mitandao ya kijamii kuchapisha taarifa za kutangazwa kwa
Baraza hilo huku baadhi ya wananchi wakitumiana ujumbe mfupi wa simu
kuhusu taarifa hizo.
Taarifa
ya mtandao wa Matukio UK, iliyosema tayari Rais Jakaya Kikwete,
ametangaza Baraza la Mawaziri juzi usiku na kuingiza sura mpya na baadhi
za waliomo sasa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, ameteuliwa kuongoza Wizara ya Uchukuzi.
Hata
hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alikanusha taarifa
hizo akieleza kwamba Baraza la Mawaziri haliwezi kutangazwa kwenye
mtandao.
Balozi Sefue alisema hana habari kuwa Rais Kikwete ametangaza Baraza la Mawaziri.
Alipoambiwa
kuwa habari hizo zimesambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Balozi Sefue
alisema: “Hiyo (mitandao ya kijamii) wala sihusiki nayo. Hayo mambo ya
mtandao siwezi kuyajibia. Baraza la Mawaziri halitangazwi kwenye
mitandao. Vuteni subira tu.”
Kwa upande wake, Jeshi la Polisi limeahidi kufuatilia taarifa hizo kwa kuwa ni sawa na uhalifu wa mtandao (cyber crime).
Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso, alisema jana kwa ufupi kwamba: "Ngoja tufuatilie."
Aidha,
Baraza hilo feki halikutaja Naibu Mawaziri na hata baadhi ya sura mpya
zilizodaiwa kuteuliwa na Rais siyo wabunge kama Katiba inavyotaka, huku
ikiacha kutaja Mawaziri walioteuliwa kuongoza baadhi ya wizara kama ile
ya Uwezeshaji na Uwekezaji, ambayo imeachwa wazi kwa madai kuwa waziri
wa sasa amehamishiwa wizara nyingine.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo ya mtandao, sura mpya ni pamoja na Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Baramagamba Kabudi
na Profesa Paul Mbawala, ambao hawana sifa za kuteuliwa kushika wadhifa
huo kwa kuwa siyo wabunge kwa mujibu wa Katiba.
Katika
taarifa hiyo, Kabudi ameteuliwa kuongoza Wizara ya Elimu wakati Profesa
Mbawala amepelekwa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Sura
nyingine mpya ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk.
Asha-Rose Migiro, ameteuliwa kuongoza Wizara ya Afrika Mashariki na
Samuel Sitta, amehamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Wengine
walioteuliwa kwa mujibu wa taarifa hiyo na Wizara zao kwenye mabano ni
Bernard Membe (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Profesa
Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), January Makamba (Kilimo, Chakula
na Ushirika), Dk. Harrison Mwakyembe (Tamisemi), Dk. Abdallah Kigoda
(Fedha), Profesa Mark Mwandosya (Utumishi), Aggrey Mwanri (Ujenzi), Dk.
John Magufuli (Maliasili na Utalii), Charles Kitwanga (Mifugo na Uvuvi
na Dk. Charles Tizeba (Mambo ya Ndani).
Wengine
ni Dk. Mary Nagu (Viwanda na Biashara), Profesa Jumanne Maghembe (Maji)
na Profesa Anna Tibaijuka (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi).
0 comments:
Post a Comment