KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa, amekana na kusisitiza kuwa hajawahi kuwasiliana na
Mwenyekiti wa chama hicho, Wilaya ya Temeke, Joseph Patrick ili
kumshinikiza ajiuzulu uongozi.
Akizungumza na MTANZANIA mjini
Dar es Salaam jana, Dk. Slaa alisema taarifa zinazotolewa na Patrick
kuwa viongozi wakuu wa chama hicho walimlazimisha ajiuzulu nafasi yake,
baada ya kubainika kumuunga mkono Zitto, ni za uongo zenye lengo la
kupotosha ukweli wa mambo. Alisema siku zote chama chake hakina utaratibu wa kufanya kazi moja kwa moja na wilaya kwa namna yoyote ile.
“Nimeshangazwa na uzushi na uongo unaosambazwa na Patrick, kwamba
sisi viongozi wa juu tulimshinikiza ajiuzulu… napenda kuhakikisha kwamba
katibu mkuu huwa hafanyi kazi na wilaya… hizi ni hila zilizopandikizwa
tu,” alisema Dk. Slaa.
Alisema yeye kama mtendaji mkuu wa chama, hajawahi kufanya mawasiliano yoyote na kiongozi wa wilaya kuhusiana na jambo lolote.
Alisema
kwa taratibu zilizopo, katibu mkuu huwasiliana na viongozi wa kanda au
mkoa ambao ndio wenye mamlaka kikatiba kufanya mawasiliano ya kikazi na
wilaya za chama.
Alisema hata kama kuna maagizo ambayo yanatakiwa
kufika wilayani, anachoweza kufanya yeye ni kuagiza kanda au mkoa ambao
wanaweza kushughulikia masuala ya ngazi za wilaya.
“Si kweli
uongozi wa chama taifa uliwahi hata mara moja kumwelekeza kiongozi
yeyote wa ngazi ya wilaya kufanya jambo au uamuzi wowote, mimi ni
muumini wa Katiba nazijua taratibu.
“Taarifa zilizoandikwa katika
vyombo vya habari zilipotosha ukweli, uongozi wa chama taifa hauna
wajibu kikatiba kufanya mawasiliano ya kikazi moja kwa moja na wilaya,
tunachoweza kukifanya ni kuwasiliana na kanda au mkoa ikibidi.
“Ni
bahati mbaya huyo anayesema mimi katibu mkuu na mwenyekiti (Freeman
Mbowe), tulimlazimisha aitishe vikao vya kujiuzulu, hasemi ilikuwa lini
na wapi, anaishia kutoa shutuma tu zisizo na ushahidi, mwambieni
awaonyeshe hizo barua na nyaraka zinazomtaka kujiuzulu, nadhani hizo ni
hila zinatengenezwa.
CHANZO; MTANZANIA