ALIYEKUWA Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba,
amekishitaki chama hicho kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, akitaka
mwongozo kuhusu mgogoro unaokitafuna.
Mwigamba amemwomba msajili atoe
mwongozo kutokana na kipengele cha ukomo wa madaraka ndani ya katiba ya
chama hicho kubadilishwa.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa CHADEMA, aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, ambaye ni mbunge wa
Kigoma Kaskazini na aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo,
walivuliwa nyadhifa zao.Mwigamba jana aliwasilisha malalamiko ofisi ya
msajili akisema katiba ya CHADEMA ya mwaka 2004 kipengele 5.3.2 (C)
inatamka kiongozi aliyemaliza muda wa uongozi ana haki ya kugombea na
kuchaguliwa tena, ilimradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kwa
muda usiozidi vipindi viwili katika cheo kimoja kwa ngazi moja.
“Hata
hivyo katiba ya chama ya mwaka 2006 kipengele cha 6.3.2 (C)
inayozungumzia muda wa uongozi kimebadilishwa na sasa kiongozi
aliyemaliza muda wake ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena ilimradi
awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi,” alisema.Alisema
sentensi kuhusu ukomo wa uongozi haipo, kwani hata katika marekebisho ya
katiba yaliyofanyika mwaka 2006 hayakuwa na mjadala wa kipengele
kilichojadili kuhusu suala zima la ukomo wa uongozi.“Si kweli kwamba
CHADEMA haijawahi kuwa na katiba ambayo ina ukomo wa uongozi, pia si
kweli kwamba mwaka 2006 katiba mpya iliandikwa upya bali marekebisho
yalifanywa kwa baadhi ya vipengele na kipengele kilichohusu ukomo wa
uongozi hakikujadiliwa,” alisema.Kwa mujibu wa Mwigamba, anatumaini
msajili atatoa mwongozo ili suala hilo lipatiwe suluhisho la kudumu
ndani ya chama hicho.Katika hatua nyingine, akizungumza na waandishi wa
habari juzi,
Albert Msando, ambaye ni mwanasheria wa Zitto, alisema
mbunge huyo amewasilisha utetezi kwa mujibu wa katiba na kanuni za
uendeshaji za chama hicho, baada ya kupokea barua yenye mashitaka 11
Desemba mosi, mwaka huu, iliyomtaka ajitete kwa maandishi.Msando alisema
licha ya kuwasilisha utetezi, Zitto ametoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa
CHADEMA, Dk Willibrod Slaa, akieleza nia ya kukata rufani Baraza Kuu la
chama hicho, kupinga hatua ya Kamati Kuu kumvua nyadhifa zake.
Alisema
kwa mujibu wa katiba na kanuni za uendeshaji, alitakiwa kabla ya
kuchukuliwa hatua angepewa mashitaka kwa maandishi na mamlaka husika na
kupewa nafasi ya kujibu kwa maandishi jambo ambalo halikufanyika.
Msando
alisema Zitto hahusiki na vurugu zozote zinazoendelea ndani ya chama
hicho, pia aliwaomba wanachama kuwa watulivu, wavumilivu na waendelee
kuwaheshimu viongozi wao wa kitaifa.