Nyumba tano kuchomwa moto, wizi wa mali na watu
kupigwa, ni sehemu ya matukio yaliyotokea katika vurugu za kutisha
katika Mji wa Ubaruku wilayani hapa, Mbeya, juzi jioni.
Vurugu hizo zimekuja baada ya wakazi wa eneo hilo
kukasirishwa na kifo cha mtoto wa umri miaka 14 anayedaiwa kupigwa na
walinzi wa mwekezaji wa Kampuni ya Mbarali Estates.
Nyumba zilizochomwa ni za mlinzi mkuu wa
kampuni, Atanas Pelela, mgambo wa kituo kilichomo ndani ya kampuni,
Ramadhani Mwamuli na ya Ofisa Uhusiano wa kampuni, Ignasi Mgao.
Pia nyumba ya Edison Joseph ambaye hana uhusiano
na kampuni, lakini hivi karibuni alihama kisiasa kutoka Chadema na
kujiunga na CCM,jambo ambalo alisema anahisi kuwa ni kiini.
Nyumba ya mtu aliyetambuliwa kuwa ni Mafikiri
Mwanishuri ilipigwa mawe na kupasuliwa vioo vya madirisha na yeye
mwenyewe kujeruhiwa na sasa amelazwa katika Hospitali ya Ikonda,
wilayani Makete.
Hata hivyo polisi wamefanikiwa kudhibiti vurugu hizo na watu 50 wanashikiliwa.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 12:00 jioni na
habari za awali zilisema vurugu hizo ziliwalenga zaidi walinzi
wanaodaiwa kumpiga na hatimaye kusababisha kifo cha mtoto Lusajo
Anosisye (14).
Mtoto huyo anadaiwa kupigwa na kujeruhiwa sehemu
mbalimbali na inasemekana kitendo hicho kilifanyika Oktoba wakati
akikatisha kwenye eneo la kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa habari hizo baada ya kupigwa mtoto
huyo alilazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali hadi alipofariki
dunia juzi jioni. Maziko yalitarajiwa kufanyika jana.
Diwani wa Kata ya Ubaruku, George Mbillah, alithibitisha tukio hilo huku akibainisha kwamba mtoto alipigwa Oktoba 29 mwaka huu
Mbillah alisema taarifa za awali zilisema mtoto
huyo alipigwa baada ya kupita kwenye njia inayokatisha eneo la shamba
wakati akipita kwenda kukata matete porini .
Inadaiwa baada ya kipigo hicho, mtoto huyo
alichukuliwa na mkurugenzi wa shamba hilo na kumpeleka kituo cha polisi
na kudaiwa mwizi .Kwa mujibu wa habari hizo, polisi walimpeleka
mahabusu katika Gereza la Rujewa.
Diwani huyo alisema mtoto huyo aliwekewa dhamana,lakini
alipotoka aliendelea kuumwa na baadaye kupelekwa katika Hospitali ya
Rujewa ambako alifariki juzi.
Baada ya habari kuhusu kifo cha mtoto huyo, wananchi walitaharuki na kuamua kuchoma moto nyumba.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwan Athuman, alisema watu 50 wamekamatwa wakihusishwa na tukio hilo.
-Mwananchi