ALIYEKUWA Mlinzi mkuu (bodyguard) wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame,
Luteni Joel Mutabazi, ametekwa na kikosi cha Jeshi la Uganda na
kukabidhiwa kwa Serikali ya Rwanda. Taarifa za kiintelijensia zinasema
kuwa Luteni Mutabazi, alikuwa akiishi nchini Uganda kwa hati maalumu ya
ukimbizi ya Umoja wa Mataifa, baada ya kutoroka nchini Rwanda pamoja na
aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo, Faustin Kayumba Nyamwasa.
Luteni Mutabazi alitorokea nchini Uganda Oktoba 2011, baada ya kutoroka jela yenye ulinzi mkali wa kijeshi ya Kami nje kidogo mwa mji wa Kigali akituhumiwa kwa kuhusishwa na kutoroka kwa mkuu huyo wa majeshi na kukimbilia Afrika Kusini. Alikuwa mlinzi mkuu wa Rais Kagame mpaka mwaka 2010, alipotoroka na kukimbilia Uganda.
Luteni Mutabazi alitorokea nchini Uganda Oktoba 2011, baada ya kutoroka jela yenye ulinzi mkali wa kijeshi ya Kami nje kidogo mwa mji wa Kigali akituhumiwa kwa kuhusishwa na kutoroka kwa mkuu huyo wa majeshi na kukimbilia Afrika Kusini. Alikuwa mlinzi mkuu wa Rais Kagame mpaka mwaka 2010, alipotoroka na kukimbilia Uganda.
Mlinzi huyo pia anashutumiwa na Serikali ya Rwanda kwa kutoa siri kwa Kikosi Maalumu cha Umoja wa Mataifa chini ya Majeshi ya Umoja ya Kulinda Amani nchini Kongo, (MONUSCO) na kuwezesha kuchakazwa na kushindwa kwa kikosi cha waasi wa M23.
Kutokana na tukio hilo, hivi sasa Serikali ya Rais Yoweri Museveni, imelazimika kumsimamisha kazi Mkuu wa Intelijensia wa Jeshi la Polisi, Joel Aguma, ambaye alihusika kumteka na kumkabidhi Luteni Mutabazi kwa Serikali ya Rwanda.
Hatua hiyo ya Aguma ilitafsiriwa kuwa ni mkakati wa kutii amri ya Serikali ya Rwanda, ambayo ilitoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa mlinzi huyo.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Rwanda imekiri kumkamata Luteni Mutabazi na kuzuiliwa katika jela maalumu ya kijeshi ya nchi hiyo mjini Kigali.
Msemaji wa Polisi wa Rwanda, Damas Gatare alisema kuwa huo ni mpango endelevu wa Serikali za Rwanda na Uganda wa kukabiliana na maasi na majasusi kutoka sehemu mbalimbali duniani na kuwa sheria itachukua mkondo wake.
Serikali ya Rwanda imesema kuwa Luteni Mutabazi, atashitakiwa kwa kosa la ujasusi na uhaini na hakuna mtu yeyote nchini humo ambaye atafanikiwa kuukimbia mkono wa sheria ambapo jeshi la nchi hiyo linaendelea kuwasaka watu hao.
Hata hivyo, Mkuu wa Polisi nchini Uganda aliyesimamishwa kazi anadaiwa kuhusika katika utekaji huo wa kumrudisha Rwanda, Luteni Mutabazi, Oktoba mwaka huu, baada ya kuhudhuria kozi ya mwaka mmoja ya makamanda iliyofanyika katika kituo cha Polisi cha Rwanda, ambapo aliibuka mwanafunzi bora katika kozi hiyo.
Mlinzi huyo alitekwa Agosti 20, mwaka huu, saa 11 jioni kutoka hotelini kwake alipokuwa katika harakati za kutaka kutumia mtandao wa Skype, ambapo alikuwa anataka kutoka chumbani kwake na kwenda sebuleni ili aweze kupata wireless intaneti.
Akiwa katika harakati hizo, ghafla walivamia makomandoo watano wa Jeshi la Rwanda wakiwa na bunduki za AK 47.
Tukio la kuvamia makomandoo hao lilizua taharuki ambapo Luteni Mutabazi, aliweza kupambana nao hali iliyowafanya makomandoo hao kushindwa kumtia nguvuni.
Makomandoo hao wa Rwanda walipoona wameshindwa kwa kupata kipigo, waliweza kutoa ishara ya kuomba msaada kwa wenzao wa nje waliokuwa katika gari.
Baada ya kuongezeka kwa nguvu kwa makomandoo hao, walifanikiwa kumvamia na kumfunika kwa nguvu kwa kitambaa kilichokuwa kimepakwa dawa hali iliyosababisha kupoteza fahamu kwa mlinzi huyo wa zamani wa Rais Kagame.
Habari za kiitelijensia kutoka nchini Uganda zinasema kuwa Luteni Mutabazi alichukuliwa kwa gari maalumu lenye namba za usajili UAK 551B na kukimbizwa hadi mpakani mwa nchi ya Rwanda ambapo alikabidhiwa kwa majeshi la Serikali ya nchi hiyo.
-Mtanzania