Meneja wa Bohari ya Dawa Kanda ya Ziwa na waandishi watatu wa habari, wamenusurika kufa baada ya gari walilokuwa wakitumia katika msafara Rais Jakaya Kikwete, mkoani Geita kupinduka.
Ajali hiyo ilitokea jana asubuhi katika eneo la
Nyankumbu katika Kata ya Kalangalala na ilihusisha gari aina ya Toyota
Land Cruiser.
Ajali hiyo ilitokea muda mfupi kabla ya msafara wa Rais Kikwete kuanza safari kuelekea wilayani Nyang’wale.
Walionusurika katika ajali hiyo ni mwandishi Peter
Fabian wa Gazeti la Rai, Frederick Katulanda wa Mwananchi, Peter
Makunga wa Radio Free Afrika na Meneja wa MSD Kanda ya Ziwa, Byekwaso
Tabura pamoja na dereva wa gari hilo Yungi Mkwati.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Tabura alisema
chanzo cha ajali hiyo ni utelezi katika eneo la lami iliyokuwa umewekwa
juu ya tuta la barabara ya moramu inayoendelea kujengwa.
Alisema hali hiyo ilisababisha gari kupoteza mwelekeo na kupinduka.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Geita, Dk Adam
Sijaona, alieleza kuwa watu hao walichunguzwa na kuruhusiwa kuendelea na
shughuli zao.