Waziri Mkuu, amesema Serikali kupitia polisi
inaendelea kujipanga kukabiliana na matishio mbalimbali ya usalama,
ukiwamo ugaidi.
Akitoa hoja ya kuahirisha Bunge Dodoma jana, Pinda
alisema matukio ya hivi karibuni nchini Kenya na kukamatwa kwa
watuhumiwa nchini ni ishara kwamba ugaidi hauna mipaka unaweza kutokea
nchi yoyote.
Pinda alirejea matukio ya kukamatwa kwa vijana 12
waliokuwa wakifanya mazoezi msituni mkoani Mtwara na wale waliokamatwa
Wilaya ya Kilindi, Tanga, kuwa ni ushahidi unaotoa wajibu wa kuimarishwa
kwa ulinzi na kuchukua tahadhari dhidi ya matukio hayo.
“Kila kiongozi wa eneo ajue watu wanaoishi katika
himaya yake. Kazi hii itasaidia kuepuka tatizo la wageni wasiojulikana
au wahamiaji haramu,” alisema Pinda.
na kuongeza:
“Aidha kamati za Ulinzi na Usalama za mitaa na
vijiji zinahimizwa kutekeleza mkakati wa kuzuia uhalifu kwa kuimarisha
vikundi vya ulinzi shirikishi, kwa kuzingatia sheria ya serikali za
mitaa na sheria ndogo zilizotungwa ili kuimarisha usalama katika
halmashauri husika”.
Alisema Serikali imekuwa ikiwahimiza
wafanyabiashara wasaidiane na vikundi vya ulinzi shirikishi huku wale
wenye biashara kubwa zenye mikusanyiko ya watu wengi wanaagizwa kufunga
kamera za usalama na kuziunganisha kwenye mtandao wa polisi ambao
wanaweza kutoa msaada pale uhalifu unapotokea.
Mpango wa BRN
Waziri Mkuu Pinda alisema Serikali imeanzisha
vitengo vya ufuatiliaji katika Wizara zote sita zinazosimamia
utekelezaji chini wa Matokeo Makubwa sasa (Big Results Now – BRN) na
kwamba mfumo huo utakuwa ukitoa taarifa za utekelezaji za kila wiki na
kila mwezi.
Alisema katika utekelezaji wa miezi mitatu ya
mwanzo yamepatikana matokeo katika sekta ya Kilimo ambako miradi 26 ya
umwagiliaji kwa wakulima wadogo imetekelezwa, pia ukarabati wa maghala
26 ya mpunga kati ya 39 yanayotumiwa na wakulima katika maeneo
yaliyopewa kipaumbele hususan katika eneo la SAGCOT.
Aliitaja sekta nyingine kuwa ni Nishati ya Umeme
ambako wateja wapya 27,494 wameunganishwa na kupatiwa umeme, ikiwa ni
asilimia 18.3 ya lengo la kuunganisha wateja wapya 150,000 hadi mwishoni
mwa 2013/2014.
“Vipande vya bomba la gesi 20,491 vinavyotosheleza
ujenzi wa kilomita 243.8 za Bomba la Gesi tayari vimewasili nchini, na
uchomeleaji wa bomba hilo kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam umekamilika
kwa Kilomita 124.3. vilevile, Kilomita 447 za njia ya bomba la gesi
zimesafishwa,”alisema Pinda.
Katika Sekta ya Elimu alisema shule za msingi 5,916 zilipatiwa
mitihani ya marejeo na mazoezi na kwamba mafunzo kazini kuhusu
ufundishaji yametolewa kwa walimu katika shule 1,325 sawa na asilimia 65
ya lengo la shule 2,048.
“Kwa upande wa huduma za maji, wananchi wapatao
752,000 waishio Vijijini wamepatiwa huduma ya maji. Mafanikio haya
yanafanya idadi ya Wananchi waishio Vijijini ambao wanapata majisafi na
salama kufikia takribani Milioni 15.9,”alisema Pinda na kuongeza:
“Kasi hii ya upanuzi wa huduma za Maji Vijijini
imewezekana baada ya Wizara ya Maji kugatua madaraka ya usimamizi wa
miradi husika kwa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, jambo
ambalo limewafanya Watendaji kuwajibika na kuharakisha utendaji wao wa
kazi”.
Bunge limeahirishwa hadi Desemba 3 mwaka huu litakapokutana katika Mkutano wa 14 mjini Dodoma