Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013, huku kukiwa
na ushindani wa maeneo mawili ambayo baadhi ya wabunge walionyesha
hofu.
Muswada huo ulipelekwa bungeni kwa hati ya dharura
kutokana na makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo yaliyofanyika
Oktoba 15, mwaka huu, baina ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa vyama
vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, baada ya muswada wa awali kususwa
na vyama vya upinzani bungeni.
Katika mjadala ulioanza juzi na kuhitimishwa jana,
wabunge wengi kutoka pande zote; CCM na upinzani waliyaunga mkono
mapendekezo ya Serikali, lakini kulikuwa na hofu kuhusu idadi ya wajumbe
watakaoteuliwa na Rais kuingia kwenye Bunge Maalumu na suala la ukomo
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Marekebisho hayo yameiweka kando Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, ambayo haitakuwapo baada ya kukabidhi rasimu ya
pili ya Katiba hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete, Desemba 15, mwaka huu.
Uhai wa tume hiyo ni miongoni mwa mambo yaliyozua
ubishi baina ya wabunge wa Kambi ya Upinzani waliokuwa wakitaka iendelee
kuwapo na wale wa chama tawala na Serikali, ambao walitaka iondoke kwa
maelezo kwamba haitakuwa na kazi baada ya kukabidhi rasimu kwa rais kama
inavyoeleza sheria ya kuanzishwa kwake.
Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu
akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani alisema kuvunjwa kwa tume
kutaathiri utekelezaji wa vifungu vingine vya sheria hivyo, ikiwa ni
pamoja na kile kinachotaka Mwenyekiti wa Tume, makamu wake au makamishna
kuitwa kwenye Bunge la Katiba kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa mambo
yatakayozua utata.
Kwa msingi huo kambi hiyo ilipendekeza tume hiyo
isivunjwe na wajumbe wake waingie katika Bunge Maalumu la Katiba kama
wataalamu wa kulisaidia Bunge hilo, lakini wasiwe na haki ya kushiriki
uamuzi kwa maana ya kupiga kura.
Hata hivyo, mapendekezo hayo na mengine ya aina
hiyo yaliyoletwa na nyaraka za marekebisho (schedule of amendments)
wakati Bunge lilipoketi kama kamati kupitia muswada huo vifungu kwa
vifungu yalitupwa, hivyo kuweka ukomo wa Tume ya Warioba mara baada ya
kukabidhi rasimu ya pili kwa Rais Kikwete, Desemba 15, 2013.
Wakati wakivutana, Lissu aliwarushia lawama
wabunge wa CCM kuwa wanawakataa wajumbe wa tume kwa sababu ilipendekeza
serikali tatu ambazo wao hawazitaki.
Lissu alisema kwa kauli na vitendo hivyo,
vilionyesha wazi kuwa CCM kinamsaliti Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph
Warioba ambaye amefanya kazi kubwa na ya weledi kiasi cha kupongezwa na
Rais Kikwete.
Katika majibu yake kwa wabunge, Waziri wa Katiba
na Sheria, Mathias Chikawe alipinga na kueleza kuwa hata kama wabunge
wangetaka Tume ya Warioba iwe ni sehemu ya Bunge la Katiba, hakuna
umuhimu huo.
Chikawe alifafanua kuwa sheria inaeleza wazi kuwa kipindi cha uhai wa tume hiyo kinakoma baada ya kukabidhi rasimu tu.
Bunge la Katiba
Kulikuwa na hoja iliyotaka wabunge watakaoteuliwa
na raia kutoka katika makundi idadi yao iongezwe hadi 292, kutoka
wajumbe 201 waliokuwa wamependekezwa.
Itakumbukwa kuwa Serikali ilishaongeza idadi hiyo
ambayo awali ilikuwa ni wajumbe 166 hadi kufikia wajumbe 201 ambao hata
hivyo bado baadhi ya wabunge walipinga kuwa ni wachache.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alitoa
hoja hiyo na kueleza sababu za kutaka idadi hiyo ambapo alisema kuwa
makubaliano ya awali yalikuwa ni lazima kuwepo na theluthi mbili ya
wabunge hao.
“Awali pendekezo la Serikali lilikuwa ni kupata
mbili ya tatu ya wabunge wote, mheshimiwa mwenyekiti, ikiwa sasa wabunge
wa Bunge la Jamhuri pamoja na Wawakilishi tunafika jumla yetu 438,
Serikali haioni kuwa mbili ya tatu ni watu 292 ni kwa nini wasikubali
wazo letu,” alihoji Mnyika.
Hoja hiyo ilileta mvutano huku wabunge kutoka
Chama Cha Mapinduzi wakilalamikia kuwa kuongeza idadi ni sawa na
kuongeza gharama za bunge.
Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba
alisema kuwa kinachompa wasiwasi Mnyika ni kutokana na ukweli kuwa
wanaotakiwa kushiriki bunge hilo wengi wanatoka Chama Cha Mapinduzi.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu, Ester
Bulaya (CCM), alipinga pendekezo la Mnyika na kudai kuwa halikuwa na
mashiko yenye masilahi kwa Taifa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokizungumza
Mheshimiwa Mnyika hakina mashiko kwani suala la kuongeza idadi ya
wajumbe halipaswi kuingizwa, sisi tuliomo humu ndani tumechaguliwa na
wananchi wote sawa na hao anaopendekeza Mnyika, kwani shida ni nini
tena?” alihoji Bulaya.
Wasomi na wanasheria wanena
Akizungumzia hatua hiyo iliyopitishwa na Bunge,
Mkuu wa Chuo Kikuu Huria, Profesa Tolly Mbwete alisema uamuzi huo
umezingatia busara na utasaidia kuepusha wajumbe wa Bunge la Katiba
kulazimishwa kukubaliana na mawazo yaliyopo kwenye rasimu.
Alisema kuwa ni vyema wajumbe hao wakaingia ndani
ya Bunge hilo kwa ajili ya kutoa ufafanuzi au maelezo pale itakapobidi,
lakini wasishiriki kama wajumbe wa Bunge hilo.
“Naona uamuzi huu umefanyika kwa busara, kwani wajumbe wa tume
tayari wameshatoa mawazo yao endapo wataingia pia kwenye Bunge la Katiba
kuna hatari ya kulazimisha mawazo hayo kupitishwa na hatimaye kuandika
kwenye Katiba ila endapo watahitajika kutoa ufafanuzi waruhusiwe
kuingia.”
Naye Profesa Abdalla Safari ambaye ni mwanasheria
alisema hakuna sababu ya wajumbe hao kuingia kwenye Bunge la Katiba kwa
kuwa mawazo yao wameshayatoa kwenye rasimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alisema uamuzi huo
haukupaswa kupitishwa kwa kuwa wajumbe wa Tume ya Warioba ndio
walioandaa rasimu, hivyo walipaswa kushiriki katika Bunge hilo kwa ajili
ya kuiwasilisha na kuitolea ufafanuzi.
Aliongeza kuwa Serikali haina mamlaka ya
kuuwasilisha muswada huo kwa kuwa tume hiyo ilichaguliwa kuwawakilisha
wananchi, hivyo kutoshiriki katika Bunge hilo kunawanyima haki ya msingi
Watanzania ambao ndiyo wanahusika na katiba hiyo.
“Tume ya Warioba inasimama badala ya wananchi
kuwanyima haki ya kushiriki katika Bunge hilo kunamaanisha kuwatoa
wawakilishi wa wananchi ambao wana uwezo wa kusimamia na kutolea
ufafanuzi wa rasimu ambayo itatengenezewa Katiba ya Tanzania,” alisema
Dk Bisimba.