OFISA UHAMIAJI ATIWA MBARONI KWA KOSA LA KUMTUKANA RAISI KIKWETE..



OFISA Uhamiaji katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), SGT Stanslausi Zacharia (37), anatuhumiwa kumtolea lugha chafu za matusi Rais Jakaya Kikwete.
 
Kwa mujibu wa chanzo chetu ndani ya Jeshi la Polisi, ofisa huyo alimtolea lugha ya matusi Rais Kikwete, Oktoba Mosi mwaka huu, eneo la Kwa Wasomali nje kidogo ya mji wa Bomang’ombe wilayani Hai.
 
Kabla, ofisa huyo anadaiwa kumtolea lugha ya matusi mhudumu wa baa moja katika eneo hilo ijulikanayo kama G.5 baada ya kuwasilisha bili ya vinywaji ambavyo alikuwa amekunywa na marafiki zake.
 
Taarifa zinadai kuwa baada ya kumtolea matusi ya nguoni mhudumu, ofisa huyo aliendelea kutoa matusi hadi kwa Rais Kikwete, tukio ambalo liliwakera wananchi na kutoa taarifa kituo kikuu cha polisi cha Bomang’ombe kisha akatiwa mbaroni.
 
Baada ya kukamatwa, alishikiliwa kwa siku mbili kwa mahojiano kisha jeshi hilo mkoani Kilimanjaro lilitoa rai kwa Idara ya Uhamiaji mkoa kumchukulia hatua za kinidhamu ofisa wake.
 
Ofisa huyo tayari amefunguliwa jalada la uchunguzi namba BNG/IR/3498/2013 katika kituo hicho cha Bomang’ombe kwa kosa la kutoa lugha ya matusi, lakini suala hilo limefanywa siri na mamlaka husika.
 
Alipoulizwa Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Johanes Msumule, licha ya kukiri kutokea aliomba lisiandikwe kwenye vyombo vya habari kwa kile alichodai watalitolea taarifa siku za usoni.
 
Akizungumza na Tanzania Daima mwishoni mwa wiki, Msumule alisema kuwa suala hilo wanalifanyia kazi kwa mapana na marefu, na kwamba tayari yuko jijini Dar es Salaam kikazi kwa ajili ya kulishughulikia.

Source:- Tanzania Daima