Golikipa
hodari nchini, Juma Kaseja jana(Novemba 08,2013) amesaini Mkataba wa miaka
miwili na klabu ya Yanga SC kwa Shilingi Milioni 40.Kaseja amesainshwa na vigogo wa Usajili wa Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb na Seif
Ahmed ‘Magari’ mbele ya Meneja wake, Abdulfatah Salim Saleh Ilala mjini Dar es
Salaam.
Kaseja sasa anakwenda kuungana na makipa wawili aliowahi kufanya nao kazi Simba SC, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deo Munishi ‘Dida’.
Hii inakuwa
mara ya pili Kaseja kusajiliwa Yanga, baada ya awali kusajiliwa mwaka 2009
akitokea Simba SC ambako baada ya msimu mmoja wa Mkataba wake kumalizika
akaachwa na kurejea Msimbazi.
Kaseja aliachwa Simba SC mwishoni mwa msimu kwa madai kiwango chake kimeshuka na amelazimika kuukosa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Bara, ingawa sasa baada ya kumwaga wino Yanga anarudi kazini Januari.
Kikubwa kilichoisukuma Yanga SC kumsajili kipa huyo ni uzoefu wake katika michezo ya kimataifa na inataka inufaike naye katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Juma Kaseja
aliibukia sekondari ya Makongo, Dar es Salaam ambako aliitwa timu ya vijana
chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys mwaka 2001 chini ya kocha Mnigeria,
Ernest Mokake aliyekuwa akisaidiwa na mzalendo, Juma Matokeyo, wote sasa
marehemu.
Mwaka huo huo alisajiliwa na Moro United aliyoichezea hadi mwaka 2003 alipohamia Simba alipopiga kazi hadi 2009 akaenda Yanga na kurejea mwaka mmoja baadaye ambako alifanya kazi hadi mwishoni mwa msimu uliopita alipotupiwa virago.