IKULU YA TANZANIA YAKIRI KUTOJUA KAMA MAWASILIANO YA RAISI KIKWETE YAMEKUWA YAKICHUNGUZWA NA MAREKANI



WAKATI Serikali ya Marekani ikiwa bado inapona majeraha ya mgogoro wa kidiplomasia na nchi washirika wake wa karibu barani Ulaya kutokana madai ya kufuatilia mawasiliano ya viongozi wa mataifa hayo, Ikulu ya Jijini Dar es Salaam imesema haijui kama mawasiliano ya Rais Jakaya Kikwete pamoja na viongozi wengine hapa nchini yanafuatiliwa na Marekani. 
 
Tamko hilo la Ikulu limekuja wakati tayari hali ya mashaka imetawala kwa viongozi pamoja na watu wa kada mbalimbali hapa nchini, kwamba ushirika wa karibu uliopo kati ya Tanzania na Marekani unaweza kuwa ni kigezo cha taifa la Marekani kufanya udukuzi wa mawasiliano yao.

Ni kutokana na hali hiyo, RAI Jumapili lilimtafuta Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, ambaye alisema: “Ikulu haijui lolote kama mawasiliano ya Rais Kikwete yanafuatiliwa, labda waulizeni wao...kwa ushauri tu nawaombeni muandike mambo ya msingi, kwa hiki mnachokifanya sidhani kama ni sahihi”.

Gazeti la RAI , wiki iliyopita liliripoti juu ya kuwepo kwa hali hiyo ya shaka, kutokana na urafiki wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na Marekani, ambapo kwa nyakati tofauti, marais watatu wa taifa hilo kubwa duniani wamepata kuzuru nchini.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Profesa John Nkoma, alipotafutwa na gazeti la  RAI kuhusiana na taarifa hizo, si yeye wala wasaidizi wake walioweza kupatikana mara moja, licha ya gazetila RAI  kutumia mbinu mbalimbali kuwafikia.

Kwa takribani wiki tatu sasa, Marekani imejikuta katika mzozo mkubwa wa kidiplomasia na baadhi ya mataifa ya Ulaya, baada ya kuibuka madai kuwa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, simu zake zimekuwa zikifuatiliwa kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.

Kauli tofauti ambazo zimepata kutolewa ndani ya wiki iliyopita na majasusi wa mataifa makubwa duniani, ikiwemo Marekani na Uingereza, wakati wakizungumzia madai ya Marekani kufuatilia mawasiliano ya Kansela Merkel, kwamba nchi zote duniani zinachunguzana, ndiyo ambayo ilijenga shaka kwamba Tanzania huenda ikawa kwenye orodha hiyo ya kufuatiliwa.

Kwa mujibu wa majasusi hao, waliozungumza na Shirika la Habari la NBC kwa sharti la kutotajwa majina yao, nchi zote duniani zinachunguzana na kwamba kinachodaiwa kufanywa na Marekani si cha kushangaza.

Kauli hiyo ndiyo ambayo baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wanadai kuwa Tanzania bila shaka haiwezi kukwepa kufuatiliwa na majasusi wa Marekani, ambao hufanya hivyo kwa nia ya kujiridhisha usalama na urafiki uliopo baina yao.

Mbali na hilo, kauli iliyowahi kutolewa na mfanyakazi wa zamani wa shirika la kijasusi la Marekani la NSA, Edward Snowden, kwamba ujasusi huo wa Marekani haufanywi dhidi ya watuhumiwa wa ujasusi na wakazi wa nchi zenye ugomvi na Marekani tu, bali hata marafiki na waitifaki wa karibu kabisa na nchi hiyo, ndiyo ambayo inajenga mazingira ya Tanzania nayo kuwemo kwenye orodha hiyo ya kufuatiliwa.

Marais watatu wa Marekani kwa nyakati tofauti wamepata kuzuru nchini, wawili kati yao ni kabla na baada ya kuondoka madarakani.

Marais hao ni Bill Clinton, George W. Bush na Barack Obama.

Bill Clinton, aliyezuru nchini mwaka 2000, wakati huo akiwa Rais, George W. Bush mwaka 2008, wote kwa pamoja kwa nyakati tofauti na kwa zaidi ya mara moja wamepata kutembelea nchini kabla na baada ya kuondoka madarakani.

Kwa upande wake, Rais wa sasa, Barack Obama, alitembelea nchini Julai mwaka huu na kuiacha Kenya, nchi ambayo ni asili yake.

Ni kutokana na hilo, hulka ya vyombo vya usalama vya Marekani kutaka kujiridhisha usalama kwa viongozi wao haiwezi kuwatenga na suala zima la kufanya udukuzi wa mawasiliano katika nchi ambazo viongozi wake wanatembelea au kutembeleana.

Kwa muktadha huo, tayari baadhi ya wachambuzi waliozungumza na RAI  kwa sharti la kutotajwa majina yao, wanasema kuwa uwezekano wa Marekani kufuatilia mawasiliano ya viongozi wa hapa nchini, akiwemo Rais wa sasa, Jakaya Kikwete ni mkubwa na ni jambo lisilo la kushangaza.

Wachambuzi hao wanazilinganisha taarifa za sasa za udukuzi wa mawasiliano unaodaiwa kufanywa na Marekani na mchezo ambao ulipata kufanywa huko nyuma na mtandao wa Weakleaks dhidi ya Tanzania.

Mtandao huo umepata kuwagusa viongozi wa serikali, akiwemo Rais Jakaya Kikwete, ukitoa taarifa za siri ilizodai kuzinukuu kutoka kwa baadhi ya maofisa wa Ubalozi wa Marekani nchini.

Juni mwaka huu, mwanausalama aliyeasi wa Marekani, Edward Snowden, alitoboa siri ya idara za usalama nchini humo kwamba zimekuwa zikifuatilia mawasiliano ya simu na barua pepe kwa watu mbalimbali duniani kote, wakiwamo viongozi wenye ushirika wa karibu na taifa hilo.

Hata hivyo, Marekani imekana kufanya udukuzi kwa namna ambayo imetafsiriwa na baadhi ya washirika wake na badala yake imedai kuwa udukuzi ambao imekuwa ikiufanya ni wa kawaida kwa ajili ya usalama na kwamba wamekuwa wakirejesha taarifa zote kwa nchi husika.

Mkurugenzi wa Idara ya Usalama ya Marekani, James Clapper, wiki iliyopita alikaririwa akisema upelelezi wa Marekani katika mataifa ya kigeni huwa haufanywi kiholela.