Kanali Makenga alizoea kutembea na bakora, ishara
kuwa alikuwa mfugaji na pia kamanda wa kijeshi aliyetaka majeshi yake
kuwa na nidhamu na kumtii.
Mrefu na mwembamba , Makenga alikulia katika
maeneo ya milimani mkoani Kivu Kusini ndani ya Jamhuri ya kidemokrasi
ya Congo, na alisifika sana kwa kuwa mlenga shabaha na mtu mwenye
maarifa na mwenye ujuzi wa kupanga mambo ya kijeshi.
Alipata ujuzi wake wa kijeshi nchini
Rwanda, ambako alikuwa mmoja wa wapiganaji wa Rais Paul Kagame kabla ya
kuchukua mamlaka mjini Kigali.
Baadaye alirejea DR Congo na kuwa mtu mashuhuri
katika harakati za kudai haki za wenyeji wa Tutsi wa Congo ambao pia ni
wachache.
Maisha ya Kanali Makenga kama mwanajeshi yalifana sana wakati wanajeshi wa M23 walipoteka mji wa Goma , Mashariki mwa DR Congo.
Pia alimshinda hasimu wake wa kijeshi ndani ya M23 Kanali Bosco Ntaganda – na kumwondoa kama kamanda wa wapiganaji wa M23.
Ntaganda alikimbilia nchini Rwanda ambako alijisalimisha kwa ubalozi wa Marekani.
Sasa yuko katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, akisubiri kufunguliwa mashitaka ya uhalifu wa kivita.
Ikiwa hatafanikiwa kukubaliana na serikali ya DRC, Makenga huenda na yeye pia akafikishwa ICC.
Ingawa hakuna kibali cha kumkamata, baraza la
usalama la Umoja wa Mataifa lilimwekea vikwazo vya usafiri pamoja na
kupiga tanji mali zake, mwaka jana likimtuhumu kwa kuongoza uasi wa M23
na kuwafanyia ukatili raia wa Congo, Mashariki mwa nchi.
Lakini kulingana na kanali Makenga, alipigana vita halali akitetea haki za jamii ya watutsi.
Mwaka huu wote kumekuwa na tetesi kua yuko
katika hili mbaya ya kiafya na kujisalimisha kwake ni ishara kuwa huenda
asirejee tena vitani.