HII NDIO AJALI ILIYOUA WALIMU WAKUU WA 3 WA SHULE ZA MSINGI


WALIMU wakuu watatu waliotajwa kuwa ni Margaret Kimbo, Agrey Kikwesha na Lanford Muhando kutoka shule mbalimbali za Tarafa ya Magole wilayani Kilosa, wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali.

Mbali ya vifo vya walimu hao, ajali hiyo iliyotokea baada ya tairi moja ya nyuma kupasuka, imesababisha majeruhi 17, baadhi yao wakiwa katika hali mbaya.

Walioshuhudia waliliambia gazeti hili kuwa ajali hiyo mbaya ilitokea juzi, majira ya saa 12 jioni katika Kijiji cha Mvumi na Rudewa, eneo la Kisangata mkoani hapa.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Magole, Koletha Mhululu, walimu hao walikuwa wakisafiri kwenda wilayani Kilosa kuitika wito wa ghafla wa mkuu wa wilaya hiyo kwa jambo la dharura ambalo hawakulifahamu mapema.

Mwalimu Koletha alisema tairi la gari hilo  lilipasuka na kusababisha lipinduke  mara nne na kusababisha baadhi yao kupoteza maisha hapo hapo.

"Tulikuwa walimu na waratibu zaidi ya 17 tukielekea wilayani kuitika wito wa mkuu wa wilaya, gari lilikuwa kasi na lilipopasuka tairi,  lilibilingika kama mara nne hivi,” alisema mwalimu huyo kwa uchungu na kushindwa umalizia.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alisema ajali hiyo ilitokea baada ya gari aina ya Toyota Hiace kupasuka tairi la  nyuma.

TANZANIA DAIMA