INAWEZEKANA umeshalizwa na mengi, umesikitishwa na vingi lakini stori
ya dada Aziza Athumani (21), anayefanya biashara ya kuuza mwili wake, inatia uchungu sana
Aziza anayefanya biashara ya kujiuza jijini Dar es Salaam kwa sasa ni
mgonjwa lakini analazimika kuendelea na biashara hiyo ili aweze kujikimu.
Sasa, hebu fuatilia mahojiano yetu na Aziza.
Ijumaa: Hebu tuambie...ni nini hasa kilikusukuma kuingia kwenye biashara hii haramu?
Aziza:
Maisha
kaka yangu, maisha. Nilizaliwa Mtwara miaka 21 iliyopita. Niliishi na
mama na wadogo zangu. Baba yangu anaishi hapa Dar. Bahati mbaya,
baadaye mama alifariki dunia. Hapo ndipo maisha yalipoanza kuwa magumu.
Ijumaa: Kwa hiyo shughuli ya kujiuza ulianza hukohuko Mtwara?
Aziza:
Hapana. Maisha yalivyokuwa magumu baada ya mama kufariki, niliamua kuja
Dar kutafuta maisha. Nilifikia kwenye baa moja iliyopo Sinza, nakumbuka
ilikuwa mwaka 2010, nikiwa na miaka 17. Kipato kilikuwa kidogo sana lakini wateja walikuwa wakiniachia chenji ndogondogo.
Ijumaa: Kwa siku ulikuwa unaweza kuingiza shilingi ngapi?
Aziza:
Hadi 10,000 nilikuwa nafikisha, wakati mwingine inazidi kidogo. Tatizo
wanaume wa baa siyo wastaarabu. Wakilewa wanaanza kukushikashika. Mimi
nilikuwa mdogo kwa hiyo nilivyokataa, nilifokewa na meneja. Nikawa
nawaachia.
Siku moja, mteja mmoja akanitaka, nikakataa.
Ikawa kama wameambiana. Karibu wote waliokuwa wakiniachia chenji
wakanitongoza, wote nikawakataa, kuanzia hapo wakawa hawaniachii chenji
tena. Maisha yakabadilika.
Ijumaa: Yakawaje?
Aziza: Nikawa sina fedha za kutosha kujikimu
mimi na wadogo zangu. Wakati mwingine nilikuwa nalala mwenyewe geto
(chumbani), wenzangu wote waliondoka na wateja (kulala nao kwa kujiuza).
Nikiwaomba pesa, wananicheka, wakaniambia na mimi nitoke.
Nikajaribu...kumbe nilikuwa naingia kwenye moto (analia)...nikajikuta
nimezoea mchezo wa kujiuza.
Ijumaa: Usilie tafadhali, tulia. Baada ya hapo ikawaje sasa?
Aziza:
Niliona biashara ya kujiuza inalipa zaidi kwa hiyo nikaamua kuachana na
baa na kujikita moja kwa moja kwenye uchangudoa. Siamini kama mimi ni changudoa lakini sitaki kabisa hii kazi, ni shida tu kaka.
Ijumaa: Pole sana...vipi kuhusu baba yako? Halafu huo mguu una tatizo gani? Pia unaweza kueleza kidogo kuhusu elimu yako?
Aziza: (analia sana – zilipita dakika tano akiendelea kulia. Juhudi za kumbembeleza zilizaa matunda baada ya muda huo).
Ijumaa: Najua inauma sana. Jipe moyo. Unaweza kuendelea sasa!
Aziza: (anafuta machozi) Huyo baba...mzee
Athumani ndiyo chanzo cha matatizo haya yote! Mimi sijasoma, niliishia
darasa la saba tu. Lakini nikasema nitajitahidi angalau niwasomeshe
wadogo zangu ndiyo maana nikaja mjini na kujikuta nimeishia kwenye
biashara ya kujiuza.
Kuna tukio ambalo siwezi kulisahau. Ilikuwa
Jumamosi, saa 9 usiku, mwezi wa saba, mwaka 2011. Mimi na rafiki yangu
Asha tulikuwa tumetoka kujiuza Kinondoni. Tulikodisha pikipiki moja,
tukapanda kwa mtindo wa mshikaki. Kwa bahati mbaya, tulipofika Magomeni
tukapata ajali mbaya. Asha na dereva walikufa palepale...Mungu amrehemu
rafiki yangu Asha (analia tena...).
Nikapelekwa Muhimbili, Kitengo cha Mifupa
(MOI), nikalazwa kwa siku kadhaa. Mguu wangu ulikuwa umeharibika sana na
hivi unavyoona nina vyuma. Niliporuhusiwa hospitalini, nikaenda kwa
baba yangu mzee Athumani, Tandika. Cha ajabu, aliponiona nina magongo,
akanifukuza akisema, eti mimi siyo mwanaye. Nililia sana, lakini kwa
sababu nilikuwa
na akiba kidogo nikaamua kurudi nyumbani kwangu Tandale nilipopanga
chumba kimoja.
Pesa ilivyoisha, nikalazimika kurudi tena
mtaani kujiuza na hii hali yangu ya magongo. Maisha haya! Sijui kwa nini
inakuwa hivi jamani!
Ijumaa: Pole sana dada. Hebu tuambie...unakutana na changamoto gani katika kazi yako?
Aziza: Nyingi lakini kubwa ambayo sitaweza
kuisahau ni kubakwa na wanaume watatu kwa mpigo, tena nikiwa na magongo
yangu. Iliniuma sana. Wanadamu wana roho mbaya sana. Nilikutana na kaka
mmoja, tukakubaliana angenipa shilingi 5,000 kwa muda mfupi.
Akasema, hana pesa ya kwenda gesti hivyo
tukaenda kwenye Uwanja wa Urafiki, Shekilango. Nikashangaa nimekutana na
wenzake wawili, nilipokataa, walinitolea kisu, ikabidi nikubali tu.
Niliumia sana siku hiyo (analia – waandishi wanambembeleza).
Tukio
lingine ni pale nilipokutana na mwanaume mmoja mwenye asili ya India,
akanidanganya na kuniambia nimzalie mtoto, nikabeba mimba yake.
Akanikana.
Huwezi amini kaka zangu, hapa nina mtoto
mdogo, hata miaka miwili hajafikisha na nilianza kutoka na kuendelea
kujiuza, mtoto akiwa na miezi mitatu tu. Mungu anamnusuru mwanangu,
anaendelea vizuri.
Ijumaa: Kwahiyo kwa sasa unafikiri nini juu ya changamoto hizi za maisha yako? Bado unaendelea na shughuli hii?
Aziza: Uongo dhambi kaka, bado najiuza lakini
nikipata mtaji wa biashara na matibabu nitaacha. Natakiwa kurudi tena
MOI mwezi wa pili mwakani kwa ajili ya kuondolewa vyuma, nimeambiwa
niende na laki tatu.
Kama umeguswa na kisa cha Aziza na unataka kumsaidia kwa hali na mali, wasiliana naye moja kwa moja kwa namba 0714 021105.
-GPL