Uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
umempelekea Zitto Kabwe taarifa ya kikao cha Kamati Kuu kilichomvua
madaraka yake ndani ya chama hicho ili aweze kukata rufaa.
Habari za kutoka ndani ya Chadema zinaeleza kuwa
Kamati Kuu ya chama hicho ilifikia uamuzi huo wakati wa vikao vyake
vilivyofanyika kati ya Januari 3 na 4, mwaka huu.
Kutokana na uamuzi huo, Zitto sasa ataweza kukata rufaa ya kupinga kuvuliwa madaraka kwenye Baraza Kuu la chama hicho.
Taarifa zinaeleza kuwa kamati hiyo ilimwagiza
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kumpatia mwenendo wa kikao
Zitto ili aweze kukata rufaa.
Dk Slaa alithibitisha jana kuwa chama hicho tayari
kimetuma muhtasari wa kikao hicho kwa Zitto, ambaye alikuwa anauhitaji
hadi kufikia hatua ya kufungua mashtaka mahakamani.
Mwanasheria wa Zitto, Albert Msando alisema wamepokea barua hiyo na walikuwa wanajiandaa kukata rufaa.
“Ni kweli tumepokea taarifa ile na tulikuwa tuna
fursa ya kuchagua kukata rufaa au la, lakini tumeisoma na tumeona tukate
rufaa,” aliongeza Msando.
Alisema hatua hiyo, bado haitasimamisha kesi
inayoendelea mahakamani, bali walalamikiwa sasa wana fursa ya kuitisha
kikao cha Baraza Kuu na kupima kama wana haja ya kuendelea na kesi.
Gazeti hili limeshuhudia barua hiyo iliyotumwa kwa Zitto, Januari 20, 2014 ikiwa na namba ya kumbukumbu namba C/HQ/ADM/KK/08/40.
Katika barua hiyo, Zitto aliarifiwa kuwa Kamati
Kuu ya Chadema katika kikao chake cha Januari 3 na 4, 2014 kiliandaa
taarifa kamili ya mwenendo wa shauri lake.
“Kwa kuwa Kamati Kuu ilikuwa ikitambua umuhimu wa
yeye kupewa nakala za mwenendo huo wa uamuzi wa kikao hicho, ilimwagiza
Katibu Mkuu wa Chadema kumpatia Zitto nakala za mwenendo wa kikao.
Barua hiyo inaeleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa
baada ya taarifa ya Zitto iliyoeleza nia yake ya kukata rufaa dhidi ya
uamuzi wa Kamati Kuu, wa kumvua nyadhifa zake.
Zitto alivuliwa nyadhifa zake na Kamati Kuu ya chama hicho,
Novemba 21, mwaka jana kwa kosa la kushiriki katika kupanga njama za
kuhujumu chama hicho.
Alivuliwa madaraka pamoja na makada wengine,
aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa
zamani wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, ambao
walituhumiwa kuhusika na kuandaa waaraka uliokuwa na lengo la kuvuruga
uongozi wa chama hicho.
Wote watatu walipewa siku 14 za kujieleza ili
wasitimuliwe kutoka kwenye chama hicho, lakini Zitto aliamua kukata
rufaa kwenye Baraza Kuu wakati wenzake hawakukata rufaa na matokeo yake
wakavuliwa uongozi Januari 6, mwaka huu.
Zitto alifungua shauri Mahakama Kuu akiitaka
kuushinikiza uongozi wa chama hicho kumpa taarifa ya kikao kilichomvua
madaraka ili akate rufaa kwenye Baraza Kuu.
Pingamizi Mahakama Kuu
Katika hatua nyingine, Chadema wamewasilisha
pingamizi la awali lenye sababu sita kwenye Mahakama Kuu wakiiomba
iitupilie mbali kesi iliyofunguliwa na Zitto.
Zitto katika kesi yake anaiomba mahakama izuie
chama hicho na wakala wake, na vyombo vyake vya uamuzi kumchukulia hatua
zozote wala kumjadili kuhusiana na uanachama wake, hadi hapo rufaa
anayokusudia kuikata Baraza Kuu la chama hicho kupinga kuvuliwa
nyadhifa, itakaposikilizwa.
Pia anaiomba Mahakama Kuu imwamuru Katibu Mkuu wa
Chadema ampatie mwenendo na taarifa za kikao cha Kamati za kumvua
nyadhifa zake zote ndani ya chama na iwazuie walalamikiwa kumwingilia
katika utekelezaji wa majukumu yake kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Mawakili wa Chadema, Tundu Lissu, Peter Kibatala
na John Mallya wamewasilisha pingamizi zao za awali kwa njia ya
maandishi juzi Mahakama Kuu wakiiomba iitupilie mbali kesi hiyo kwa
sababu haina msingi na gharama zilipwe na Zitto walitoa sababu sita.
Katika sababu ya kwanza, mawakili hao wanadai kuwa
shauri hilo halina msingi kwa vile halikuwahi kusikilizwa kwenye
mahakama ya chini.
Sababu ya pili wanaiomba mahakama iitupilie mbali
kwa vile imewasilishwa kwenye masijala kuu ya Mahakama Kuu badala ya ile
ya wilaya.
Wanadai katika sababu ya tatu kuwa kesi hiyo haina
msingi kwa kuwa mlalamikaji hajaomba maoni ya Mahakama Kuu kuhusiana na
suala lake la uanachama wa Chadema.
Nne, wanadai kuwa anaendesha mashauri mawili ya kukata rufaa ili
kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema kwa wakati mmoja, jambo ambalo
ni matumizi mabaya ya mahakama.
0 comments:
Post a Comment