Rais Kagame Wa Rwanda Anusurika Kufa....Atangaza Kuacha Urais, Uingereza yatakiwa kukata misaada



RAIS wa Rwanda, Paul Kagame amenusurika kifo baada ya msafara wake nchini Kenya kupata ajali na kusababisha watu wawili kujeruhiwa vibaya. 

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), imeelezwa kuwa ajali hiyo ilihusisha mojawapo ya magari ya msafara wake nchini Kenya, alipokuwa kwenye ziara za kikazi.

Hata hivyo, Rais Kagame hakujeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea saa mbili asubuhi jana eneo la Limuru nchini Kenya. Dereva wa gari hilo alipoteza mwelekeo katika barabara kuu ya Nairobi-Limuru, hata hivyo gari hilo lilikuwa mbali na msafara wa rais huyo. Aidha majeruhi wa ajali hiyo walikimbizwa haraka hospitalini.

Rais Kagame alikuwa anarejea mjini Nairobi kutoka katika kongamano la Magavana wa Kenya mjini Naivasha katika Bonde la Ufa.

Kagame alialikwa kuhudhuria kongamano la Magavana nchini Kenya, kuhusu uongozi mzuri na utawala bora.

 

***Nataka kuacha Urais

Akihutubia Magavana hao, Kagame alisema anatamani kuacha nafasi ya urais hata kabla ya muda wake kumalizika mwaka 2017, kwani dhamira yake inamlazimisha kufanya hivyo.

Alisema anataka kuanza kujishughulisha na masuala ya elimu na si siasa tena.

Alieleza kuwa wakati wa harakati za kuikomboa nchi hiyo mwaka 1980, hakuwahi kufikiri kama angekuwa rais wa nchi hiyo, lakini kitendo cha kufanikiwa kuchukua nafasi kubwa ya kisiasa ndani ya nchi hiyo, lilikuwa ni jambo zuri.

“Nilikuwa na mipango mingine ambayo sikudhani haya yangetokea. Nataka kutoka ili nishiriki kwenye masuala ya elimu na kuachana na siasa kabisa,” alisisitiza Kagame.

Kagame alisema kwamba: “Nilitaka kuwaonesha kwamba kwanini nipo katika nafasi hii sasa, si kwamba nilifanikiwa kwa kuandika barua ya maombi.”

Aliongeza kuwa ushiriki wake ndani ya kikundi cha NRA, ulisababisha ushindi kwa kikundi hicho mwaka 1986 na baadaye mapambano yakaelekea Rwanda.

“Niliipigania Uganda kwa muda wa miaka mitano na Rwanda kwa muda wa miaka minne. Sikuwa kwenye handaki, sikufikiria kuwa Rais wa Rwanda.

“Nimepigania maisha na uhai, vitu vilihusishwa kwa namna vilivyokuwa kila kimoja kilifuata kingine,” alisema.

Aliongeza kuwa wakati akiwa kwenye vita na kikundi cha RPF na baadaye kukawa na mazungumzo ya amani jijini Arusha mwaka 1990, wengi walisema atakuwa rais.

Akizungumzia mazingira ya siasa ndani ya nchi yake, Kagame alisema anaitafsiri katika dhana mbili, kwanza huwezi kufanya kila kitu. Vyote hivi vinakuonesha namna ulivyo na hilo ni kwa kila mmoja sio kwangu tu, kwani mazingira yamenifanya niishi kama jiko la mvuke.

Kagame alitoa ushauri kwa viongozi wa Serikali, kushirikiana vema na watu wanaowaongoza ili kukuza maendeleo ya nchi zao kwa muda mfupi na mrefu.

Alisema Rwanda imefanikiwa kupiga hatua haraka kimaendeleo, kwa sababu watu wake waliogopa kurudi kule walikotoka awali. Kauli hiyo ya Kagame inaonekana kuwa ni mbinu ya kumaliza tofauti za kisiasa zinazoikumba nchi yake kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Mjadala mkubwa unaoendelea sasa ndani ya nchi za ukanda wa Maziwa makuu, ni kuona kama Kagame atakubali kuachia madaraka hayo au atasubiri mabadiliko ya Katiba ili kumuongezea muda wa kuwania nafasi hiyo.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa mambo ya kisiasa, wamesema kuwa Kagame anataka kufuata nyayo za aliyekuwa Rais wa Kenya, Daniel Arap Moi, Jerry Rawlings wa Ghana na Joachim Chissano wa Msumbiji, ambao waliheshimu muda waliotakiwa kukaa madarakani, kwani walikaa kwa muda wa miaka 15. Hotuba hiyo aliyoitoa juzi, aliwataka magavana kuwahusisha wananchi katika uamuzi wa maendeleo.

Uingereza yatakiwa kukata misaada Rwanda

Wakati huo huo Serikali ya Uingereza, imetakiwa kukata misaada kwa Serikali ya Rwanda hadi hapo uchunguzi wa vifo vyenye utata ambavyo vinadaiwa kusababishwa na Serikali hiyo utakapofanyika.

Kauli hiyo imetolewa juzi na Waziri Kivuli wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Jim Murphy, kwa Serikali ya Uingereza ili kuokoa maisha ya wapinzani wa Serikali ya Rwanda iliyopo madarakani.

Uingereza ambayo hutoa msaada wa euro milioni 90 kila mwaka kwa Serikali ya Rwanda, imedai kufedheheshwa na matukio yanayoendelea kuhatarisha usalama wa wananchi wa Serikali hiyo.

Kauli ya waziri huyo imekuja wakati ambao Polisi nchini Afrika Kusini, wakianza uchunguzi kufuatia kuuawa kwa aliyekuwa mkuu wa idara ya ujasusi ya Rwanda, Kanali Patrick Karegeya.


>>MTANZANIA

0 comments: