Mbowe kuitikisa kambi ya Zitto Kabwe...


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, leo anatarajiwa kuwasili mkoani Kigoma kwa ajili ya kufanya mikutano ya Operesheni M4C Pamoja Daima. Mbowe ambaye atafanya mikutano katika wilaya zote za mkoa huo, anatarajia kupita kwenye ngome za aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.

Hii itakuwa mara ya kwanza, Mbowe kufanya mikutano hiyo, baada ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbrod Slaa kufanya mikutano ya kuimarisha chama mwishoni mwa mwaka jana.

Katika mikutano hiyo, Dk. Slaa alikumbana na upinzani mkali kutoka kwa wafuasi wa Zitto, ambao wengi walihoji sababu za kutimuliwa kwake.
 

Lakini akionyesha msimamo, Dk. Slaa alisema kama kuna mwanachama anamtaka Zitto, basi amfuate aliko kuliko kuendelea kupoteza muda wake ndani ya chama.

Pamoja hali hiyo, wiki moja baadaye mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini, alitua mkoani humo na kufanya mikutano ambayo ilihusishwa na madai ya kujibu mapigo ya Dk. Slaa.

Katika mikutano yake, Zitto alisema katu hatorudi nyuma katika mapambano ya ujenzi wa demokrasia nchini, huku akiahidi kama kuna jambo zito atarudi kwa wananchi ili wamuelekeze nini cha kufanya.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Kigoma, Msafiri Wamaywa alisema, Mbowe atawasili saa 8 mchana akitokea mkoani Tabora kwa kutumia helikopta.

“Tunatarajia mwenyekiti wetu atawasili kesho (leo) mchana, tumepanga atahutubia mkutano wa kwanza kwenye Viwanja vya Mwanga Center,” alisema Wamaywa.

Alisema ujio wa Mbowe ni mwendelezo wa Operesheni M4C Pamoja Daima, ambayo inaendelea nchi nzima.

Alisema lengo la operesheni hiyo, ni kuwafumbua macho wananchi kuhusu mchakato wa Katiba Mpya pamoja na kuimarisha chama.

Alisema kwa mujibu wa ratiba, Mbowe atafanya mkutano wa pili katika eneo la Nguruka, kisha atakuwa na Baraza la Mashauriano la Mkoa ambalo litafanyika mjini Kasulu.
 
MPANDA
Naye, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohamed, aliwataka Watanzania kuendelea kupuuza propaganda za udini zinazoenezwa na watu wasioitakia mema Tanzania.

Akizungumza katika mikutano ya M4C- Operesheni Pamoja Daima kwa nyakati tofauti maeneo ya Sikonge (Tutuo), Mpanda Magharibi (Kalema na Mwese), Mpanda Mashariki (Majimoto) na Mpanda Mjini, alisema kama watu wataendelea kujadili masuala hayo chama chake hakitakubaliana nao.

“Wananchi tunajua mnaambiwa propaganda nyingi kweli kweli. Uzuri tunajua hata wao wanajua kuwa mmezipuuza na mmewapuuza, wamekuja na udini, ukabila na ukanda nawaambieni hatawafanikiwa sisi tunazidi kujiimarisha tu.

“Katika vitabu vitakatifu, tunaambiwa kuwa mtu hukuzwa au hufanywa kuwa maarufu na imara kupitia midomo ya wamchukiao ambao hawaishi kumsema kila wakati, ndipo CHADEMA ilipofika. Imepewa umaarufu na wanaoichukia, ambao kutwa nzima wanatunga maneno ya kutufitinisha na Watanzania, lakini wameshindwa,” alisema Mohamed.
 
MNYIKA
Naye, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema anasikitishwa kuendelea kuwapo na vitendo vya ujangili, wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda akishindwa kukemea wakati yeye ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali.

Alisema vitendo vya ujangili katika Pori la Ugara, havikubaliki hata kidogo.
 
Lema
Naye, Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amewataka vijana kuwa mstari wa mbele kuonyesha moyo wa ujasiri na uzalendo wa kupigania maslahi ya nchi yao.

Alisema taifa lolote lile, vijana ndiyo nguzo na tegemeo katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kuhoji na kutafakari mustakabali wa jamii zao, huku wakiwa mbele kufanya mabadiliko kwa ajili ya manufaa ya kizazi chao na vizazi vingine vinavyokuja.

“Wananchi wa Mpanda Mashariki, wakati ninyi kama tulivyo Watanzania wengi hivi sasa, mnazidi kudidimia katika lindi la umaskini ambao unasababishwa na uongozi mbovu na sera mbovu za chama tawala CCM, mbunge wenu ambaye ni Waziri Mkuu amekazana kuimba nyimbo na kushikilia ndoto za ufugaji wa nyuki.

“Poleni wananchi wa Mpanda, ninawaonea huruma kwa sababu hali hii ya umaskini…hamuwezi kuondokana nayo kwa sababu kiongozi wenu haoneshi dalili za kupambana na umaskini yeye mwenyewe,” alisema Lema.

>>MTANZANIA

0 comments: