Makundi ya Urais wa 2015 yanaendelea kuivuruga CCM baada ya
Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Singida, Mgana Msindai kuibuka na
kusema atamburuta mahakamani Mwenyekiti mwenzake wa Mkoa wa Geita,
Joseph Kasheku ‘Msukuma’ asipomwomba radhi kwa kumchafua kwa kumwita
mpuuzi.
Hata hivyo, Kasheku amesema Msindai anaweza kwenda
mahakamani huku akisisitiza kwamba hawezi kumwomba radhi kwa kuwa
anaamini kwamba alichofanya ni kinyume cha taratibu za chama na vikao.
Juzi, Kasheku alimponda Msindai mbele ya waandishi
wa habari kwa kitendo chake cha kusema kuwa wenyeviti wa CCM wa mikoa
yote ya Tanzania wanamuunga mkono, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
katika safari yake ya urais wa 2015 wakati wa sherehe ya mwaka mpya
huko Monduli, Arusha.
Msindai alisema jana kuwa amemtaka Kasheku aitishe
mkutano wa waandishi wa habari na kumwomba radhi. “Asipofanya hivyo
ndani ya siku saba nitampeleka mahakamani,” alisema Msindai.
Msindai pia alikanusha kuwa aliwekwa kitimoto katika mkutano wa wenyeviti wa CCM wa mikoa uliofanyika Zanzibar.
Msindai aliyekuwa Mbunge wa Iramba Mashariki kwa
miaka 15, alikiri kuwa alialikwa pamoja na wenyeviti wenzake sita katika
sherehe ya mwaka mpya iliyoandaliwa na Lowassa huko Monduli.
Katika sherehe hizo, Lowassa alitangaza kuwa
ameanza safari ya matumaini, kauli ambayo wachambuzi wa masuala ya
kisiasa waliitafsiri kama tangazo la kuwania urais mwaka 2015.
Msindai alikanusha kutangaza kuwa wenyeviti wote
wa CCM wa mikoa wanamuunga mkono Lowassa wakati wa sherehe hiyo... “Mimi
ni Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, lakini sikuwahi kuzungumza kuwa
wenyeviti wote wanamuunga mkono Lowassa katika Uchaguzi Mkuu 2015...
kikubwa tulichozungumza ni kumuunga mkono katika safari yake ya
mafanikio katika kuendeleza elimu, maji, ujenzi wa zahanati.”
Msindai alisema wanamwangalia Lowassa kutokana na
uwezo wake katika kusimamia mipango yake ya maendeleo na zaidi katika
kupigania elimu pana kwa Watanzania.
“Alipokuwa Wizara ya Maji alichangia maji
kupatikana Dar es Salaam na mikoani na maendeleo mengi, uwajibikaji
kwenye jimbo lake na aendelee hivyo...hayo ndiyo tuliyomsifia.
Nilizungumza haya na sitabadilika,” alisema Msindai, ambaye alisema
haogopi kufukuzwa.
“Mimi si mpya ndani ya CCM kama ‘Msukuma’. Nina
miaka zaidi ya 40, ninaelewa taratibu zote za chama za udiwani, ubunge
na urais. Kama ni kampeni ni baada ya chama kumpitisha mtu na sisi
tutamuunga mkono... hata mimi ninaweza kuwania urais,” alisema.
Siombi radhi
Kwa upande wake Kasheku alisema hamwombi radhi Msindai, kwani si
wenyeviti wote wa CCM wanaomuunga mkono Lowassa katika safari yake
aliyoiita ya matumaini.
“Siombi radhi na hata sasa hivi anaweza kushtaki,
tulipokutana Zanzibar alitueleza kuwa alitoa kauli ya kuumuunga mkono
Lowassa kimakosa na kusema alikuwa akimaanisha yeye na wenzake
aliokwenda nao Monduli ndiyo wanamuunga mkono Lowassa,” alisema Kasheku.
Kasheku alifafanunua kuwa Msindani alisema kuwa
wanahabari walikosea kumnukuu baada ya kuandika katika vyombo vya habari
kuwa alisema wenyeviti wote wanamuunga mkono Lowassa.
Alisema baada ya Msindai kukiri jambo hilo,
wenyeviti waliokuwa Zanzibar waliandaa tamko la pamoja na kuagiza
lisomwe na Msindai mbele ya wanahabri katika Ukumbi wa Idara ya Habari
Maelezo, Dar es Salaam.
“Katika huo mkutano ilitakiwa niwepo mimi
(Kasheku), Msindai na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan
Madabida, ila cha ajabu mwenzetu (Msindai) alitukimbia na tulipomtafuta
akasema yupo Singida, hivyo sisi tuliamua kutoa tamko lile,” alisema
Kasheku.
Alisema kauli aliyoitoa Msindai ni kinyume na
maagizo ya wenyeviti wote wa CCM, huku akimtaka kabla ya kwenda
mahakamani, ahakikishe kuwa amewasilisha malalamiko yake ndani ya chama
ili Kamati ya Maadili ya chama ikae na kutoa uamuzi.
“Hatuna ugomvi na Lowassa, tuna ugomvi na yeye
aliyetuweka nyuma yake na kusema wote tunamuunga mkono Lowassa, nani
alimwambia maneno hayo na ilikuwa katika kikao gani?,” alihoji Kasheku
na kuongeza:
“Kama kuna watu wapo nyuma ya Lowassa au mtu
yeyote ni siri yao, iweje yeye atulazimishe sisi kuwa nyuma yake kwa
mgongo wa Mbunge wa Monduli”.
Mgeja amtetea Msindai
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Hamis
Mgeja ambaye pia alikuwa Monduli, alimtetea Msindai akisema hakuwahi
kuzungumzia suala la urais katika mkutano huo wa Monduli zaidi ya
kumsifu Lowassa kwa mafanikio aliyoleta kwenye jimbo lake na maeneo
mengine alipokuwa Waziri Mkuu.
Alisema hakuna dhambi kwa kumpenda mtu yeyote,
wote wanaotoa kauli za kukanusha ni dalili za woga, wivu, kutokujiamini
na inawezekana wana watu nyuma yao.
Source:- Gazeti la Mwananchi
0 comments:
Post a Comment