Madereva bodaboda mkoani Mbeya wapora maiti kanisani na kuamua kuizika wenyewe baada ya kuchoshwa na ibada ndefu ya mchungaji....



Kundi la vijana 60, juzi walipora mwili wa marehemu Gabriel Ngalele ukiwa unaombewa kwenye Kanisa la Tanzania Assemblies Of God (TAG) eneo la Uyole jijini baada ya kuchoshwa na ibada ndefu ya mchungaji. 
 
Ibada hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Mchungaji, Edward Mtweve wa kanisa hilo ambaye alijikuta kwenye mazingira magumu baada ya vijana hao wanaodaiwa kuwa ni madereva wa pikipiki kuvamia madhabahu na kubeba sanduku lililokuwa na mwili wa marehemu.
 
Marehemu Ngatele alikuwa dereva wa pikipiki na alifariki kwenye ajali iliyotokea eneo la Sae baada ya pikipiki yake kuligonga lori lililoharibika katikati ya barabara. Katika ajali hiyo, abiria pia alifariki.
 
Mwili wa marehemu ulipelekwa katika kanisa hilo, na wakati mchungaji akiendesha ibada kulijitokeza kelele za hapa na pale na kusababisha mchungaji kuomba utulivu mara kadhaa.
 
Lakini kelele nyingi zililipuka ghafla zikiwamo za kulalamika kwamba ibada ilikuwa ndefu na hatimaye vijana wengi walionekana wakiingia kwenye mlango na kuvamia madhabahu na kutoka na mwili wa marehemu.
 
Baada ya kuuchukua mwili, vijana hao walikwenda kwenye makaburi kuuzika wakati naye mchungaji akiendelea kuhubiri waumini waliobaki ndani ya kanisa.
Mchungaji Mtweve alilazimika kwenda nyumbani baada ya kumaliza ibada badala ya makaburini, huku vijana nao wakiendelea na taratibu za mazishi kwa utaratibu uliosimamiwa na Mwenyekiti wa waendesha pikipiki Mbeya, Vicent Mwashoma.
 
Mwendesha pikipiki aliyetajwa kwa jina la Bahati Mwasote alilazimika kuendesha ibada ya mazishi.
 
Mchungaji Edward Mtweve alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema alisikitishwa na kitendo cha kuvurugwa kwa ibada.
 
 Marehemu Gabriel Osward Ngalele.
 Mchungaji Edward Mtweve wa kanisa la Tanzania Assemblies of God[TAG]Uyole.
 
 Mchungaji wa Bodaboda Bahati Mwasote

0 comments: