MBIO za kusaka urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na
uteuzi wa nafasi nne za mawaziri, vinaelezwa kukibomoa chama hicho,
Tanzania Daima limedokezwa.
Mbali na mambo hayo, mchakato wa uundwaji wa katiba mpya ambayo
rasimu ya pili imetoka hivi karibuni na kuingizwa kwa serikali tatu,
umeonekana kukiathiri zaidi chama hicho kinachotaka uwepo wa serikali
mbili.
Tayari viongozi wa CCM wameshaanza maandalizi ya kukutana na wabunge,
wawakilishi na wabunge wa Bunge la Katiba watakaochaguliwa, kwa lengo
la kuweka msimamo wa kutopitisha serikali tatu wakati wa majadiliano.
Wanataka hoja ya serikali tatu isifikishwe kwenye kura ya maoni ambako wana hofu inaweza kupata uungwaji mkono.
Hofu ya makada hao wa CCM ni kuwa muundo wa serikali tatu utabomoa
muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na Rais wa Kwanza wa
Zanzibar, Abeid Amani Karume na Julius Nyerere aliyekuwa Rais wa
Tanganyika.
Wakati suala la katiba mpya likionekana kuwaumiza vichwa makada wa
chama hicho, mbio za urais unaotarajiwa kufanyika mwakani, nazo zimezidi
kukipasua chama hicho.
Hadi hivi sasa viongozi wa CCM wamekuwa wakipambana na aliyekuwa
Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambaye katika siku za hivi karibuni
alitangaza safari ya matumaini kuelekea ndoto zake za kuwapatia
Watanzania elimu bure na huduma bora za msingi.
Lowassa, alitangaza safari hiyo iliyotafsiriwa ni ya kuwania urais
katika mkesha wa mwaka mpya jimboni kwake Monduli, ambako aliwaalika
makada mbalimbali wa CCM wakiwemo wajumbe wa vikao muhimu vya maamuzi.
Miongoni mwa waliokuwepo kwenye hafla hiyo ni Mwenyekiti wa wenyeviti
wa chama hicho, Mgana Msindai, ambaye alisema wanaunga mkono safari ya
Lowassa.
Tangu Lowassa atangaze safari yake hiyo, viongozi wa CCM, akiwemo
Makamu Mwenyekiti (bara), Philip Mangula, wamejitokeza hadharani
kumpinga.
Mangula alisema chama chake kimeunda timu ya kuchunguza makada wake
walioanza harakati za kuwania uongozi kabla ya pazia kufunguliwa, na
wakibainika kutenda kosa hawatapewa nafasi ya kuwania nafasi husika.
Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), nao ulitaka Lowassa atimuliwe kwa
madai ya kukivuruga chama na kupanga safu yake ya kuwania madaraka
ilhali Rais Jakaya Kikwete hajamaliza muda wake.
Wakati chama hicho kikionekana kupambana na Lowassa, mbunge huyo juzi
katika ukusara wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook aliandika:
“Ukiona unatumia nguvu nyingi kumchafua mtu kwa kumpakazia mambo,
kumsengenya, kumfitinisha na kumsingizia, ujue yeye ni bora kuliko wewe,
kichafu kinaonekana hata bila kuambiwa.”
Uwaziri moto
Nafasi nne za mawaziri waliotenguliwa uteuzi wao kutokana na kuguswa
na kashfa ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za ubinadamu katika
Operesheni Tokomeza Ujangili, nazo zimewafanya makada wa chama hicho
kupigana vikumbo kila kukicha.
Mawaziri hao ni Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Shamsi Vuai
Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Emmanuel Nchimbi (Mambo ya
Ndani) na David Mathayo (Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi).
Baadhi ya wabunge na mawaziri inadaiwa wamekuwa karibu na familia ya
Rais Kikwete ili wapate fursa ya kuwemo kwenye baraza la mawaziri ambalo
linatarajiwa kufanyiwa mabadiliko makubwa.
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa baadhi ya wabunge na
mawaziri wamekuwa wakitapeliwa na watu wanaojitambulisha ni askari wa
usalama wa taifa.
Inadaiwa askari hao wamekuwa wakiwaeleza mawaziri na wabunge kuwa
wamepewa jukumu la kuandika ripoti au kufanya uchunguzi juu ya mienendo
ya wahusika na ili waandike yaliyo bora huwadai fedha wahusika.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliwataka wabunge na
mawaziri wasirubunike na utapeli huo kwakuwa Rais Kikwete hajawapa kazi
hiyo.
Baraza la mawaziri hadharani
Leo huenda kiu ya Watanzania kujua nani ametoswa nani amekumbukwa
kwenye Baraza la Mawaziri ikakatwa ambapo majina yao yataanikwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana jijini
Dar es Salaam na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Sefue, leo atakutana na waandishi wa habari Ikulu.
Ingawa taarifa hiyo haikubainisha ni jambo gani litakalozungumzwa,
suala la kutajwa kwa mawaziri wapya na mabadiliko ya baraza hilo ni
jambo linalotarajiwa.
0 comments:
Post a Comment