Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imemteua Mahmoud Thabit Kombo, kuwa mgombea wa kiti cha uwakilishi katika Jimbo la Kiembesamaki.
Jimbo hilo limekuwa
wazi baada ya aliyekuwa mwakilishi wake, Mansoor Yussuf Himid, kufukuzwa
uanachama kwa madai ya kwenda kinyume na maadili na sera za CCM.
Akitangaza
uamuzi huo jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema: “Kamati Kuu imemteua Mahmoud kuwa mgombea wa CCM. Ni mgombea
aliyekidhi vigezo, ana uwezo wa kutosha, hodari, muumini wa Muungano na
mtetezi wa Mapinduzi ya Zanzibar.”
Akizungumza mara baada ya uteuzi huo, Kombo alisema anashukuru jina lake kupitishwa na kwamba anaamini CCM itashinda.
“Nafikiri
sina ubora wa kuwapita wenzangu ila kura zangu zimetosha. Nitaungana na
kushirikiana nao katika kukitafutia ushindi chama chetu. Tunajenga
nyumba moja hatutagombania fimbo,” alisema Mahmoud ambaye ni mtoto wa
aliyekuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa ASP, hayati Thabit Kombo Jecha.
Wengine
waliokuwa wakiwania kuteuliwa ni Suleiman Haroub Pandu, aliyeshika
nafasi ya pili katika kura ya maoni na Mwanaasha Abdallah, aliyeshika
nafasi ya tatu.
Wote watatu jana asubuhi walionekana wakiingia kwenye Jengo la CCM Kisiwandui wakati kikao hicho kikiendelea.
Kampeni
za uchaguzi huo mdogo zinatarajiwa kuzinduliwa Januari 22 mwaka huu na
mgeni rasmi anatazamiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk Mohamed Gharib Bilal na kufungwa Februari mosi na Mjumbe wa
Kamati Kuu ya CCM Balozi Seif Ali Idd.
Wakati huohuo, Nape alisema msimamo wa sera ya CCM wa kutetea muundo wa Muungano wa Serikali mbili bado unaendelea.
Alisema licha ya rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupendekeza Serikali tatu, msimamo wa CCM uko pale pale.
Nape
alisema msimamo wa kuwa na muundo wa serikali mbili ulitokana na sera
ya chama hicho na kwamba hadi sasa hakuna kikao chochote cha kikatiba
kilichokaa na kubadili msimamo huo unaopingana na mapendekezo ya tume.
Chanzo : Mwananchi
0 comments:
Post a Comment