Bunge la Katiba Kizungumkuti,

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba bado ina upungufu ambao utaathiri utendaji wa Bunge Maalumu, ambalo huenda likaanza Februari 11 mwaka huu, mjini Dodoma.

Sheria hiyo Namba 8 ya 2011, imeishafanyiwa marekebisho mara mbili yakiwamo ya Februari 2012 na Novemba 2013, lakini mabadiliko hayo yameacha kasoro ambazo zinapaswa zifanyiwe tena kazi, kupitia Bunge.

Kasoro zipo katika Kifungu cha 22 kinachohusu uchaguzi wa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum, pamoja na kifungu cha 24 kinachozungumzia Katibu na Naibu Katibu wa Bunge hilo wanavyoanza kutekeleza wajibu wao.

Kupitia Sheria ya Marekebisho (Na:2) ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2013, Bunge katika mkutano wa 12, liliwapa mamlaka Katibu wa Bunge na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, ‘kufanya maandalizi muhimu kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Bunge Maalumu’.

Watendaji hao kwa mujibu wa sheria ndio watakaoteuliwa kuwa Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu baada ya Rais kutangaza kuitishwa kwa Bunge hilo, lakini kiapo chao kitasubiri hadi pale watakapochaguliwa Mwenyekiti na Makamu wa Bunge hilo.

Sheria husika inaweka sharti kwamba ikiwa Mwenyekiti atatoka upande mmoja wa Muungano basi Katibu atoke upande mwingine na kinyume chake. Hivyo lazima wasubiri uchaguzi huo ili wajue ni nani Katibu na Naibu Katibu.

Kifungu cha 24 (2) kinasema: “Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu, watashika nyadhifa zao kwa misingi kwamba, endapo Mwenyekiti atachaguliwa kutoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano basi Katibu wa Bunge Maalumu atatoka upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano”.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa tayari baadhi ya wataalamu kutoka Ofisi ya Bunge na ile ya Baraza la Wawakilishi (BLW) wameanza maandalizi ya awali katika moja ya hoteli za jijini Dar es Salaam.

Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashililah mbali na kukiri kuanza kwa maandalizi hayo, hakuwa tayari kuzungumzia kwa undani suala hilo kwa maelezo kuwa lazima ashirikiane na Katibu wa Baraza la Wawakilishi. 

Hata hivyo, kutokana na mkanganyiko mkubwa uliopo katika Sheria hiyo, ni dhahiri watendaji hao watapata wakati mgumu katika kuanza kutekeleza majukumu, hasa katika kuteua wajumbe wa sekretarieti ya Bunge hilo.

Uteuzi wa wajumbe hao kwa mujibu wa kifungu cha 24 (4) unapaswa kufanywa na  Katibu kwa kushauriana na Naibu wake, nafasi ambazo hazitakuwapo hadi pale Mwenyekiti na Makamu wake watakapochaguliwa.

Fursa ya marekebisho

 

Hivi sasa hakuna fursa kwa Bunge la Muungano kufanya marekesho katika sheria hiyo ili kuondoa mkanganyiko uliopo, kwani kikao chake ambacho kilipaswa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu hadi mwanzoni mwa Februari, kilifanyika Desemba mwaka jana, ili kutoa fursa kwa  Bunge Maalumu.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki alisema jana kuwa ikiwa kuna kasoro zozote zitakazojitokeza, wataalamu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wale wa Baraza la Wawakilishi watazifanyia kazi.

“Kuwapo kwa upungufu katika sheria zinazotungwa huwa ni jambo la kawaida, lakini pili katika sheria huwezi kuandika kila kitu na ndiyo maana katika mabadiliko yaliyofanyika Katibu wa Bunge na mwenzake wa Baraza la Wawakilishi walipewa wajibu wa kisheria kufanya maandalizi,” alisema Kairuki na kuongeza:

“Na tulifanya hivyo makusudi kwani tunata uzoefu uliopo katika vyombo hivi utumike katika kuendesha Bunge la Katiba, mimi ninawaamini wataalamu wetu kwa hiyo hakuna kitakachoharibika.”

Vifungu vinavyokanganya

Kifungu cha 22 kimeweka masharti kwamba baada ya kuitishwa kwa Bunge hilo, Katibu wa Bunge la Muungano na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, watasimamia mchakato wa kumchagua Mwenyekiti wa muda wa Bunge Maalumu.

Kadhalika, kifungu cha 24 (5) cha Sheria hiyo kinasema: “ Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalum, kabla ya kushika madaraka yao wataapa au kula yamini mbele ya Rais”. Kwa maana hiyo, watendaji hao watasimamia uchaguzi wa mwenyekiti wa muda pasipokuwa  na nguvu ya kisheria kwani watakuwa hawajala kiapo kutokana na kutofahamu nafasi zao; ni yupi Katibu na Naibu Katibu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa muda ambaye anachaguliwa kwa mujibu wa Kifungu cha 22 (a) na (b), ndiye atakayesimamia uandaaji na upitishwaji wa Kanuni za Bunge Maalum na kuendesha uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo.

Lakini ni dhahiri kwamba Mwenyekiti wa muda atachaguliwa bila kuwapo kwa kanuni, huku kukiwa hakuna utaratibu wowote wa kisheria anaoelekeza jinsi atakavyopatikana.

Kadhalika kifungu cha 26 (1) cha Sheria hiyo kinataka shughuli zote za Bunge Maalum ziendeshwe kwa kufuata Kanuni husika na pia kifungu cha 24 (3) kinawataka watendaji watatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Kanuni hivyo uchaguzi wa Mwenyekiti wa muda na usimamizi wake lazima vizingatie kanuni jambo ambalo haliwezekani kwani zitakuwa hazijapitishwa.

 

0 comments: