UGANDA YAANZA KUILIPA MABILIONI TANZANIA IKIWA NI FIDIA KWA TANZANIA KWA MCHANGO WAKE KATIKA KUMUONDOA IDD AMIN DADA UGANDA MWAKA 1978....!!

SERIKALI ya Uganda tayari imeshaanza kulipa deni lake kwa Tanzania la dola za Marekani milioni 9.6 kati ya dola za Marekani milioni 18.4 ikiwa ni fidia kwa Tanzania kwa mchango wake katika kumuondoa Idd Amin Dada Uganda mwaka 1978.


Hayo yalibainishwa bungeni jana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Shamsi Vuai Nahodha, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mbinga, John Komba (CCM).

Katika swali lake Komba alitaka kujua kama Tanzania ilishaanza kudai fidia kwa Serikali ya Uganda kutokana na mchango wake wa kuisaidia nchi hiyo kumuondoa Idd Amin na kumfanya Rais wa sasa Yoweri Museveni kutawala kwa amani nchini humo.

Akijibu swali hilo, Nahodha alikiri kuwa Tanzania ilipigana vita na Uganda kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 1979 kutokana na uvamizi uliofanywa na Uganda chini ya utawala wa Idd Amin aliyevamia na kukalia sehemu ya ardhi ya Tanzania mkoani Kagera.

“Kwa kuwa vita hivyo vilitokana na uvamizi wa Idd Amin, baada ya vita kumalizika Serikali ya Tanzania iliitaka Uganda kulipa fidia. Serikali hiyo nayo ilikubali kuilipa Tanzania fidia hiyo,” alisema Nahodha.

Alisema kwa bahati mbaya Serikali ya Uganda haikutekeleza makubaliano hayo yaliyofanyika mwaka 1979 hivyo Serikali ya awamu ya tatu ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mstaafuma William Benjamin Mkapa ilifanya majadiliano tena na Uganda.

Alisema kutokana na majadiliano hayo Serikali ya Uganda ilitakiwa kulipa fidia dola za Marekani milioni 18.4 na hadi sasa Serikali hiyo imeshalipa dola za Marekani milioni 9.6 fedha ambazo ziliwekwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali na nchi hiyo kubakiwa na deni la dola za Marekani milioni 8.8.

Nahodha alisema majadiliano baina ya Tanzania na Uganda yanaendelea ili sehemu ya fidia iliyobaki iweze kulipwa chini ya Wizara ya Fedha ambayo ndio inayofuatilia deni hilo.

Akijibu swali la nyongeza la Komba la kuitaka Tanzania imkumbushe Museveni juu ya namna Tanzania ilivyosaidia nchi yake hivyo aache kuihujumu kwa kusaidiana na Rais wa Rwanda Paul Kagame, Nahodha alisema siku zote Tanzania haimsaidii mtu ili kupata shukurani. “

Tanzania ni nchi ya kipekee sana, imebahatika kupata viongozi wenye sifa kubwa duniani kama Nyerere (Mwalimu Julius), kiongozi huyu aliwahi kusema Waafrika ni ndugu na Afrika yetu sote, tuliwasaidia Uganda kwa utu hatutegemei zaidi,” alisisitiza.

Alisema hata juzi baada ya kifo cha Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Tanzania ilitoa tamko la kumuenzi kwa kusisitiza uvumilivu, jambo ambalo limeipatia sifa kubwa Tanzania. “Naomba tuendelee kuitunza sifa hii na si vinginevyo.