
Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Rose Temba, jijini Dar es Salaam jana wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutolewa uamuzi. Rufaa hiyo ilifikishwa mahakamani hapo na mawakili wa Shekhe Ponda, wakitaka kufutwa kwa shtaka la kutotii amri halali ya mahakama inayomkabili mteja wao.
Baada ya kuwasilishwa maombi hayo mahakamani hapo, upande wa Jamhuri ulidai kuwa ombi hilo ni batili kwakuwa kiapo kinachounga mkono madai yao kinakasoro za kisheria kinyume nakifungu cha nane cha sheria ya viapo.
Wakili wa Serikali,Bernard Kongola ,alidai kuwa,kutokuwepo kwa tarehe katika kiapo hicho kilichoapwa na Wakili Hamidu Ubaidi, ni makosa pia kiapo hicho hakijaeleza kama aliyeapa alifanya hivyo mbele ya wakili anayemfahamu.
Awali, wakili wa Shekhe Ponda, Juma Nassoro aliiomba mahakama kutupilia mbali pingamizi la upande wa Serikali kwa madai kuwa, halina msingi kisheria, bali ni maelezo, hivyo alitaka mahakama hiyo kuangalia ombi hilo kwa jicho la haki na si kiufundi.
Akitoa uamuzi wake jana, Jaji Temba, alisema baada ya kupitia hati hiyo aliona ina dosari zilizotajwa na upande wa Jamhuri, hivyo kutupilia mbali maombi ya Ponda kutokana na dosari zilizojitokeza. Alisema anakubaliana na hoja za upande wa Jamhuri kwani kabla alikuwa ameshaona dosari hiyo kwenye hati ya kiapo.
"Nilishangaa kuona zimeshafanyiwa marekebisho, hivyo naagiza mawakili wa Shekhe Ponda wachukuliwe sheria kali za kinidhamu na vyombo vinavyohusika " Alisema Temba
credit:-Majira