HAYA NDIO MAJIBU YA ZITTO KABWE KWA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI BAADA YA MWANASHERIA MKUU KUSEMA KUWA ZITTO NI MNAFIKI NA MUONGO..!!

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), amesema atamjibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema juu ya kauli aliyoisema bungeni kwamba mbunge huyo hana majina ya Watanzania walioficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi. Zitto alisema kwa kuwa Jaji Werema alimshambulia kupitia bunge naye atatoa majibu bungeni ili ukweli uweze kujulikana.


Zitto alitoa kauli hiyo jana nje ya ukumbi wa Bunge alipokuwa akizungumza na Rai iliyotaka kujua msimamo wake baada ya Jaji Werema kuliambia Bunge Zitto aliiambia kamati iliyoundwa na Serikali kuchunguza sakata la Watanzania wanaodaiwa kuficha fedha nje ya nchi kwamba hana majina.

“Nilimsikia Mwanasheria MKuu wa Serikali akinishambulia jana (juzi), nitakachokifanya ni kwamba wiki ijayo nitamjibu hapa bungeni baada ya kumuomba Spika anipe nafasi ya kuwasilisha maelezo binafsi.

“Mwanasheria Mkuu ni muongo, nasema totally ni muongo kwa sababu kwenye kamati yao nimehudhuria mara nne na nikawakabidhi majina ya watuhumiwa.

“Tena kibaya zaidi, niliwakabidhi mpaka jina la mchunguzi wa kimataifa anayeweza kuwasaidia katika uchunguzi wao, halafu leo anasema nilikuwa naikwepa kamati ni muongo, nasema ni muongo, lakini, hoja iliyopo ni je, mabilioni yapo au hayapo,” alisema Zitto kwa kifupi.

Juzi, Jaji Werema aliliambia Bunge jinsi ambavyo Zitto alikuwa akikwepa kutoa taarifa za watu walioficha fedha nchini Uswisi.

Jaji Werema alisema licha ya mbunge huyo kukaririwa mara kadhaa akisema anayo majina ya walioficha fedha hizo nje ya nchi lakini mara kadhaa alikuwa akikwepa kuhojiwa na kamati iliyoundwa na Serikali kufuatilia fedha hizo.

Alisema kutokana na tabia hiyo Serikali imeazimia kuchukua hatua za kisheria dhidi yake na kusisitiza hawawezi kukubali mtu alidanganye Bunge.

Jaji Werema alisema hayo alipokuwa akihitimisha mjadala wa taarifa ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala.

“Lakini leo hapa amesema Serikali haina nia ya kurudisha fedha zilizofichwa Uswisi, kwa maana hiyo Mheshimiwa Naibu Spika, Zitto Kabwe ni mzito na nakubaliana na Lema (Mbunge wa Arusha Mjini) aliyesema hapa kwamba Zitto alete majina hayo,” alisema Jaji Werema.

Source:-  Mtanzania