MBUNGE aliyeteuliwa na Rais, Dk Asha Rose Migiro ameapishwa rasmi jana bungeni na kusema anafurahi kutumikia umma huku akiahidi utumishi wenye uadilifu, uaminifu na wa kujituma.
Dk Migiro aliapishwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda jana saa tatu asubuhi baada ya kuingia bungeni akisindikizwa na wabunge .
Baada
ya kuapishwa, Dk Migiro alipongezwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Fredrick Werema na kusalimiana na Kabwe
Zitto na wengine.
Baadaye
alielekezwa kiti chake kisha Bunge likaendelea na kipindi cha maswali
ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu na yale ya kawaida.
Mara
baada ya kumalizika kwa kipindi hicho, Migiro aliyefuatana na watoto
wake alizungumza na waandishi wa habari na kushukuru kupewa heshima na
fursa nyingine kutumikia Taifa.
Alisema
mtu anaweza kufanya kazi yoyote na zote zina thamani katika maisha
lakini kutumikia umma ni heshima ya pekee kwani ukifanya kazi kwa
ufanisi basi matokeo yake yanasambaa kwa watu wengi zaidi.
“Ubunge ni utumishi kwa umma ninachoahidi kwa Watanzania ni utumishi wenye uadilifu, uaminifu na kujituma,” alisema.
Alisema
kama alivyowahi kusema siku za nyuma ukipewa fursa kama hiyo si mali
yako binafsi bali heshima kwa wanawake kwa kuongeza idadi ya wanawake
bungeni.
Migiro
alisema wanawake wana wajibu, hivyo wanapopata fursa wana kila sababu
kutumikia umma na nchi kwa moyo na nguvu na kubainishwa wazi ubunge ni
uwakilishi bila kujali wa kuteuliwa, wanawake au jimbo.
Migiro
aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) ni Katibu wa
Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayesimamia Idara ya Siasa
na Uhusiano wa Kimataifa. Migiro mwanzoni mwa mwezi huu aliteuliwa na
Rais kuwa Mbunge.